Madeni huwa hayatokei ghafla katika maisha ya kila siku. Baadhi ya matumizi husababisha madeni, hivyo ni muhimu kujua na kuwa makini na tabia zinazokupelekea kudaiwa kila wakati ili kuweza kuokoa fedha nyingi zaidi na kufanya mambo ya msingi.
Baadhi ya tabia unazotakiwa kuacha ili kupunguza na kuepuka na madeni ni hizi hapa:
- Kutumia fedha nyingi kuliko kipato chako
Siku zote matumizi huwa hayaishi hivyo ni muhimu kuwa makini kwani ni rahisi kutumia fedha zaidi ya kiasi unachoingiza kwa mwezi. Kutumia akiba, kukopa kwa watu wengine na kutumia mikopo ni baadhi ya mambo yanayoweza kusababisha madeni. Mwanzoni inaweza kuwa rahisi kwako kulipa madeni lakini itafikia kipindi yatakuelemea na kuleta changamoto kubwa. Ni muhimu kuelekeza matumizi yako kulingana na kipato ulichonacho ili kuepuka madeni yasiyokuwa na ulazima.
- Kutumia fedha ambazo huna
Kuna ile tabia ya kufanya manunuzi na kulipa kwa kutumia fedha ambazo unategemea kupata mbeleni. Kwa kufanya hivyo tayari unakuwa na deni kwa sababu kwanza huna fedha hivyo itakubidi aidha ukope, au uchukue fedha kabla ya kazi kuisha (advance) au utumie fedha katika akaunti yako huku ukijiwekea kuwa utazirudisha baada ya kupata fedha siku za mbeleni.
Hivyo basi ili kuepuka hili unatakiwa kupunguza matumizi yasiyo na umuhimu ili iwe rahisi kupunguza gharama za maisha na kuishi kulingana na kipato chako huku ukiweka bajeti ili kuwa na mfumo wa kifedha unaoeleweka.
- Kutotumia fedha taslimu
Baadhi ya watu ambao huona afadhali wadaiwe tu kuliko kutoa fedha taslimu, mara nyingi huwa hawana sababu ya maana inayowapelekea kufanya hivyo kwa sababu fedha wanakuwa nayo tayari. Ni muhimu kufanya maamuzi ambayo hayatakuletea changamoto baadae. Kopa kama kuna umuhimu wa kufanya hivyo, kama hakuna umuhimu basi weka mazoea ya kulipa kila unapohitaji huduma au bidhaa.
- Kutumia deni kulipa deni
Inatokea kuwa kuna muda unakuwa unadaiwa na huna fedha. Ni bora kuzungumza na mtu au kampuni inayokudai ili uweze kuongezewa muda wa kutafuta fedha na kulipa kuliko kukopa sehemu nyingine ili ulipe mkopo unaodaiwa. Kwa kufanya hivyo unakuwa umeongeza mzigo mwingine wa deni na hii inaweza kuleta changamoto kwako hapo baadae ikiwa mikopo itakuwa mingi. Pia unaweza usikopeshwe tena kama una historia ya kukopa na kutorudisha. Epuka kukopa ili kulipa mkopo mwingine, jitahidi kuweka mpango madhubuti kabla hujakopa ili kujua namna utakavyolipa mkopo.
Kuwa na madeni mengi kunaweza kusababisha upotevu wa mali kama nyumba, gari, kiwanja n.k. Madeni pia husababisha kupata historia mbaya ya ukopaji ambayo italeta shida kipindi unapotaka kukopa tena. Ni vyema kuwa na mpango kabla na baada ya kukopa ili kuepuka changamoto zinazoweza kuathiri mwenendo wa maisha yako.