Ni rahisi kutengeneza vikwazo unaposhindwa kufikia malengo uliyonayo lakini ukweli halisi ni kwamba, kama huwezi kupigania kile unachotaka huenda ni kwa sababu huna nia ya kufika mahali hapo. Sababu nyingi zinazopelekea kutotimiza malengo ni rahisi kutatuliwa endapo ukitulia na kutafakari kwa kina changamoto hizo kwa kuwa ni changamoto ambazo huwakuta watu wengi.
Katika makala hii, nitaeleza baadhi ya vikwazo ambavyo vinakwamisha kutimiza malengo.
Kukosa malengo maalum
Kamwe huwezi kutimiza malengo yako kama unakosa lengo maalum kutoka mwanzo. Malengo kama ‘utajiri’ au ‘kuwa na mafanikio’ sio malengo maalum kwani huna mkakati wa jinsi ya kufika huko. Kwa kuanza tafakari kwa makini malengo yako hasa ni nini. Kuwa na lengo maalum na baada ya hapo andaa mpango maalum ambao utakusaidia kutimiza lengo hilo. Kwa mfano badala ya kusema lengo lako ni kununua nyumba, sema kwamba lengo lako ni kuwa na akiba ya Sh. 10,000,000 ili kununua nyumba ndani ya miaka miwili ijayo.
Ratiba
Kama unaamka na kufanya kitu hicho hicho kila siku, biashara, ajira au mradi wako utakuwa ni sehemu tu ya siku yako kwa kuwa unakosa hamasa ya kujituma na kuleta mabadiliko. Ili kufikia malengo yako, ni muhimu kuwa na ratiba ambayo itakuongoza sio tu katika majukumu yako bali katika kutimiza malengo madogo madogo bila kukariri.
Muongozo
Kukosa muongozo sahihi ni kama kwenda mahali ambapo hupafahamu vizuri hivyo hujui njia sahihi. Wakati mwingine kuwa na mtu ambaye anakuongoza na kukushauri ni muhimu kwani unakuwa na uhakika wa muelekeo wako. Washauri ni watu muhimu katika mafanikio na kutimiza malengo kwa kuwa wana ujuzi zaidi na hivyo watakuongoza vizuri.
Uwajibikaji
Kuwa mchapakazi ni kitu kimoja lakini kuwa na moyo wa kuendelea kuhamasika kufanya kazi kwa bidii siku hadi siku ni kitu kingine. Hii hutokea hata kwa watu ambao wamefanikiwa. Wakati mwingine unakosa hamasa ya kufanya kazi hivyo unakata tamaa ya kutimiza malengo yako.
Kutojifunza kutokana na makosa
Badala ya kuvunjika moyo kwa sababu ya makosa yako, jifunze na jaribu kuepuka kuyarudia kwa mara nyingine tena. Lazima utakutana na changamoto ambazo zinaweza kukufanya ukate tamaa. Chukua changamoto hizo na zitumie kujifunza na kuwa bora zaidi ili kufika unapotaka.