Home VIWANDAMIUNDOMBINU Usafiri huu unawaangalia watu wa chini?

Usafiri huu unawaangalia watu wa chini?

0 comment 39 views

Hakuna asiyependa kusafiri ndani ya muda mfupi. Safari hii ni furaha kwani haichoshi na mtu anaweza kufika mapema na kufanya shughuli zake mara moja. Usafiri wa ndege umerahisha maisha kwa kiasi kikubwa kwani hakuna tena sababu ya kupoteza siku nzima barabarani. Lakini huduma hii haipatikani kirahisi. Watanzania walio wengi bado wanaumizwa na gharama kubwa ya usafiri wa anga. Wengi hulazimika kusafiri na magari kwani japokuwa wanachoka, wanaokoa kiasi kikubwa cha fedha.

Kwa kawaida gharama za kusafiri zinazotozwa na makampuni binafsi ni kubwa kuliko zile ambazo hutozwa na serikali. Hii nayo inatishia biashara kwa makampuni haya ambayo tayari biashara yake ni ngumu. Lakini uwepo wa shirika la ndege la serikali umesaidia kwa kiasi kikubwa kwani wanatoza gharama nafuu zaidi.

Watanzania wengi wanaangukia katika uchumi wa kati au wa chini na hivyo kutumia fedha nyingi kusafiri ni kitu ambacho kipo nje ya uwezo wao. Mashirika ya ndege yanapoanzisha huduma hizi katika nchi ambazo asilimia kubwa ya wananchi wake ni wa kipato cha chini wanapaswa kuzingatia gharama za huduma zao ili jamii inayowazunguka ipate kufurahia huduma.

Watu wenye hali ya chini kiuchumi wasiachwe nyuma katika hili. Ni vizuri kuwepo na mazingira ambayo kundi hili la watanzania nao watafaidi usafiri huu wa aina yake. Ni kweli hatuwezi kufananisha gharama za uendeshwaji wa magari na zile za usafiri wa ndege lakini inawezekana kabisa kulegeza kidogo gharama za safari ili watu wengi zaidi wapate nafasi ya kuzifurahia.

Hili likiwezekana, watu wengi zaidi watapata fursa ya kutumia huduma hizi na kwa kurahisisha usafiri, shughuli nyingine za kiuchumi kama biashara zinaweza kupelekwa sehemu mbalimbali na hivyo kusaidia kuinua pato la taifa. Vilevile gharama za usafiri wa anga zikiwa rafiki zaidi, utalii wa ndani nao unaweza kukua kwa kiasi kikubwa kwani itawezekana kusafiri kwenda katika vivutio mbalimbali vilivyopo hapa nchini kwa bei nafuu na muda mfupi.

Ni kweli kuwa sio kila mtu ataweza gharama ya usafiri wa ndege lakini kiwango cha huduma hii kikiwa rafiki zaidi kulingana na uwezo wa kiuchumi wa watu walio wengi, basi sekta ya usafiri wa anga itaimarika kibiashara kutokana na ongezeko la wateja.

Vilevile katika kuimarisha usafiri huu ni vizuri kama mashirika ya ndege yakaongeza ubunifu ili kushawishi wateja kutumia huduma zao. Mbali na hivyo pia wanatakiwa kuhakikisha kuwa wateja wao wanapata huduma bora ambayo itawavutia kurudi tena siku nyingine. Usafiri ni kichocheo kikubwa cha maendeleo katika nchi yoyote ile hivyo inatakiwa kuhakikisha kuwa gharama za kusafiri ni rafiki ili kuwawezesha watu wengi zaidi kufanya shughuli zao za kimaendeleo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter