Bila shaka mlipuko wa lori la mafuta uliotokea katika kijiji cha Itigi, Msamvu mkoani Morogoro Agosti 10 mwaka huu ni tukio ambalo limeleta simanzi kwa watu wengi. Kwa mujibu wa vyombo mbalimbali ya habari, idadi ya waliofariki hadi sasa imefikia 75 baada ya majeruhi wengine wanne waliokuwa wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kufariki dunia usiku wa kuamkia jana.
Kwa mujibu wa walioshuhudia ajali hilo, kilichopelekea tukio hilo la kusikitisha ni dereva wa pikipiki ambaye alikuwa amebeba mama na mtoto kukatisha barabarani ambapo dereva wa lori hilo lililobeba mafuta aina ya petroli kutoka jijini Dar es salaam alikuwa akijaribu kuwakwepa, lakini kwa bahati mbaya lori likapinduka.
Baada ya kupinduka kwa lori hilo, moto kubwa ulilipuka na kuua watu takribani 62 ambao walikuwa wakichota mafuta papo kwa papo. Imeelezwa kuwa walioathirika zaidi na ajali hii ni waendesha pikipiki maaraufu kama bodaboda.
“Miili iliopolewa kwenye eneo la tukio na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ili kuhifadhiwa na kubaini majina yao ni wakina nani na ufuatiliaji unaendelea. Tumefanikiwa kuuzima moto huu mkali wa petroli majira ya saa nne na nusu asubuhi hii kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa, Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na wananchi pamoja na TANESCO kwa kuzima umeme maeneo haya”. Alisema Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Wilboad Mutafungwa mara baada ya moto huo kuzimwa.
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ambaye alifika katika eneo la tukio amesema ameunda tume maalum kwa ajili ya kuchunguza kama kulikuwa na uwajibikaji wa viongozi ili hatua stahiki zichukuliwe. Majaliwa pia amehimiza wananchi kukaa mbali pindi ajali inapotokea.
“Ujumbe mmepata, si vyema kukimbilia vitu. Ajali hizo ziwe fundisho kwa watanzania. Jukumu letu sote kwanza ni kuwaombea marehemu na kuwaombea majeruhi afya njema”. Alisema Waziri Majaliwa.
Akizungumzia ajali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk. Stephen Kebwe ameeleza kuwa ajali hiyo imeleta maafa makubwa kutokana na vifo hivyo.
Naye Mbunge wa Morogoro Mjini Abdulaziz Abood ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi kuacha mazoea ya kukimbilia mahali ambapo ajali inatokea hususani magari yanayobeba mafuta.
Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli naye aliungana na watanzania wote kuomboleza msiba huu mzito. Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu, JPM ametoa pole kwa wote walioguswa na msiba na kuwaombea majeruhi.
“Nimeumia sana kusikia idadi kubwa ya watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali hii. Natoa pole kwa wote walioguswa na vifo hivi hasa familia za marehemu wote, nawaombea marehemu wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka”. Imesoma taarifa hiyo.
Pamoja na salamu za pole, Rais Magufuli naye amesisitiza tabia ya wananchi kukimbilia magari baada ya kupata ajali kukoma mara moja kwani ni hatari.
Tukio hili la kusikitisha limeacha simanzi sio tu kwa watanzania bali hata watu wengine duniani. Vyombo vikubwa vya habari vikiwemo Al Jazeera, Idhaa ya Kiswahili DW na BBC vimeungana na wananchi wa Morogoro na Tanzania nzima kuomboleza. Salamu za rambirambi zimeendelea kumiminika kwa wingi kutoka sehemu mbalimbali duniani kote kupitia mitandao ya kijamii.
Watanzania wote tunapaswa kujifunza kutokana na maumivu haya ya msiba huu. Tuache tabia ya kukimbilia katika maeneo ya ajali ili kuepusha maafa zaidi.
Tuendelee kuwaombea ndugu zetu wapumzike salama, majeruhi wapone haraka. Vilevile, tuendelee kuchangia damu kuwasaidia.
BWANA AMETOA NA BWANA AMETWAA, JINA LAKE LIHIMIDIWE.
AMEN.