Home AJIRA Unataka kuajiri kupitia intaneti? Fanya hivi

Unataka kuajiri kupitia intaneti? Fanya hivi

0 comment 109 views

Maendeleo ya kiteknolojia yanazidi kurahisisha mambo mengi katika jamii ikiwa ni pamoja na suala la ajira. Siku hizi ni rahisi kutangaza kazi na kupata mrejesho kutoka kwa watu mbalimbali kutoka sehemu za mbali baada ya muda mfupi kwa kuwa wengi wanatumia mtandao wa intaneti hivyo imekuwa rahisi kupata habari.

Mbali na watu wengi kuamua kujiajiri, ajira bado ni changamoto katika jamii zetu. Hivyo ni vyema kuwa makini ikiwa utatangaza nafasi ya kazi kupitia mtandao kwa sababu sio kila mtu ana malengo sahihi. Na wakati mwingine watu hukubali kufanya kazi au kutuma maombi mtandaoni ili hali wakijua kuwa hawana vigezo stahiki.

Hakikisha unazingatia haya:

Maarifa: Kwanza ni muhimu kuelezea vizuri ni watu wenye maarifa gani unahitaji ili kuwarahishia waombaji kutafakari kama wanaweza kazi hiyo au la. Pili waombaji wakituma maombi yao hakikisha wana ujuzi unaohitaji ili kuepukana na changamoto yoyote inayoweza kutokea kutokana na ujuzi mdogo wa mfanyakazi. Hivyo mwambie mtu unayetaka kumuajiri akutumie kazi zake za awali ili uone uwezo wake na kufanya maamuzi sahihi.

Vifaa: Kuna baadhi ya kazi ambazo hutangazwa humuhitaji muombaji kuwa na vifaa kwa ajili ya kazi hiyo. Hivyo ikiwa umetangaza kazi na unahitaji muombaji kuwa na vifaa maalumu kwa ajili ya kufanya kazi husika basi jitahidi kumuuliza muombaji kuhusu vifaa alivyo navyo na uwezo wake au kumpa kazi ya majaribio ili kupima uwezo na ubora wa vifaa vyake.

Mawasiliano: Mawasiliano ni muhimu sana ikiwa umemuajiri mtu kupitia mtandao kwa sababu kwanza mnatakiwa kupanga mipango kuhusu ufanisi wa kazi husika hivyo ni muhimu kujua kama mnaelewana kwa lugha, na majukumu anaweza kufanya. Kuwa na mawasilano mabaya mtu unaemuajiri kupitia mitandao ya intaneti kutaleta shida katika ufanisi wa kazi hivyo hakikisha una mawasiliano mazuri na mtu unayemuajiri na mna maelewano mazuri.

Mrejesho wa watu wengine: Ikiwa mtu unayetaka kumuajiri amewahi kufanya kazi na watu wengine basi ni rahisi kujua kama anafaa au vinginevyo. Hivyo unaweza kuwauliza waajiri waliopita kuhusu ufanisi wa kazi wa mtu huyo ili kufanya maamuzi sahihi na kuhakikisha kazi unayotaka ifanyike inafanyika na mtu sahihi. Kuwa makini na mirejesho hiyo pia kwani sio kila mtu atakwambia ukweli kuhusu muombaji huyo, hivyo mbali na mirejesho hiyo kwa sababu haujaona na mtu huyo basi changanua kwa umakini sifa zake na mapungufu yaliyosemwa na watu kisha fanya maamuzi ambayo hayataathiri maendeleo yako na biashara/kampuni yako.

Gharama: Siku zote ni muhimu kukumbuka kuwa ili kuendelea ni vyema kugharamia vitu kulingana na uwezo wako. Hivyo hata kwa mtu unayemuajiri kupitia mtandao hakikisha hutumii gharama ambazo ziko nje ya uwezo wako kwa sababu kwa kufanya hivyo unaweza kuathiri mtiririko wako wa fedha. Hakikisha unampata mtu mwenye uwezo wa kulidhisha kwa gharama nafuu au unayoweza kuimudu.

Kuajiri watu kupitia mitandao hupunguza gharama kwa muajiri, hivyo ni vyema kuwa makini, na kufanya maamuzi sahihi ili kuhakikisha kuwa kazi zako zinaenda sawa, kwa gharama nafuu na maendeleo yanaonekana.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter