Home FEDHA Elimu matumizi bora ya fedha changamoto kwa wajasiriamali

Elimu matumizi bora ya fedha changamoto kwa wajasiriamali

0 comment 52 views

Kukosekana kwa elimu ya matumizi bora ya fedha kumetajwa kama moja ya changamoto inayofanya wajasiriamali wengi kuwa na mikopo isiyo rasmi (mikopo umiza).

Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ally Mussa, amesema hayo wakati wa kikao na timu ya kutoa elimu ya fedha kwa umma kutoka Wizara ya Fedha ambayo ipo Mkoani Morogoro kutoa elimu hiyo kwa makundi mbalimbali ya wananchi katika halmashauri saba (7) za mkoa huo.

‘’Shida moja niliyoigundua kwa wananchi wetu wa Morogoro wanaweza wakapewa mkopo, na pengine hawana haja ya kupewa mkopo kutokana na kipato chao, lakini kipato chenyewe kinatumika vibaya na kikitumika vibaya inawasababishia kuwa na mikopo isiyotarajiwa hasa ile ya kinyonyaji’’ amesema Dkt. Mussa.

Amewataka wajasiriamali wa Mkoa huo kuwa na matumizi bora ya fedha wanazozipata katika shughuli zao mbalimbali za uzalishaji mali ili kuepukana na mikopo isiyo rasmi (mikopo umiza).

Dkt. Mussa amewataka waratibu wa program ya elimu hiyo pamoja na yale waliyokusudia kuwaelimisha wananchi kuhusu program ya utoaji elimu ya masuala ya fedha, wakumbuke pia kuwaelimisha kuhusu matumizi ya rasilimali walizonazo ambazo zitawasaidia kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi na hatimaye kuwaepusha na mikopo ya kinyonyaji.

Amewaasa wananchi wa Halmashauri zitakazotembelewa na timu kuhakikisha hawakosi fursa hiyo ya kupata elimu ya masuala ya usimamizi wa fedha binafsi, uwekaji wa akiba, mikopo na mengineyo ambayo itawasaidia katika maisha ya baadaye.


Awali akizungumza kwenye kikao hicho, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha Bw. Stanley Kibakaya, amesema kuwa lengo la Wizara kutoa elimu hiyo ni kuwahimiza wananchi wa Mkoa wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla kuhakikisha pesa wanayoipata kutokana na uzalishaji mbalimbali wanaoufanya wanaiwekeza kwa ajili ya matumizi ya baadae.

Aidha, Kibakaya ameongeza kuwa program ya elimu ya fedha italenga pia watoa huduma ya fedha kwa kuwahimiza kutoa huduma hizo kwa kufuata sheria na miongozo iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Taasisi ambazo hazijajirasimisha kufanya hivyo ili wapatiwe leseni itakayowawezesha kufanya shughuli za utoaji wa huduma ndogo za fedha kwa kuzingatia sheria.

Katika Tarafa ya Mikese wananchi wamesema kuwa elimu inayotolewa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha nchini imekuwa na msaada mkubwa.

Wananchi hao wamesema wamesumbuka kwa muda mrefu kutokana na baadhi ya watu wasio waaminifu kutoroka na fedha zao walizokuwa wanawekeza kupitia vikoba visivyo rasmi.

Katika shuhuza zao, wanaeleza kuwa wamekuwa wakijiunga katika vikundi mbalimbali ili waweze kupata fedha ama kwa kukopa au kwa kujiwekeza, lakini kwa kupitia vikundi hivyo kuna watu ambao sio waaminifu wanatoroka na fedha na kuwafanya wapate hasara jambo linalosababisha kuzorota kwa ukuaji wa uchumi wao.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Fulwe, Kata ya Mikese Sarah Stwati, amesema kuwa amekuwa akipokea kesi nyingi kuhusu waweka hazina wa baadhi ya vikundi kuondoka na pesa za wanachama hivyo anaamini kupitia elimu hiyo itakuwa mkombozi kwa wananchi wa kijiji cha Fulwe na Tarafa nzima ya Mikese katika suala zima la uwekezaji.

Kwa upande wake, Afisa Usimamizi wa Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, Jackson Mushumba amesema kuwa umuhimu wa utoaji elimu kwa wananchi ni kuhakikisha wanaachana na mikopo umiza pamoja na kuwa na uelewa kuhusu taasisi zinazotoa mikopo na vitu vya kuzingatia wakati wa kuchukua mkopo.

Mushumba ameongeza kuwa Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha nchini wanaendesha program ya elimu ya fedha kwa kutumia nyenzo mbalimbali za kufundishia elimu hiyo, ambapo kwa Tarafa ya Mikese wameamua kutumia nyenzo ya filamu ambayo ni rafiki kwa wananchi kwa sababu kupitia filamu wataelimika na kuburudika.

Program ya elimu ya fedha kwa umma inalenga kujenga uelewa na weledi kwa umma katika matumizi sahihi ya huduma za fedha zinazotolewa ili kujenga Uchumi na kuondoa umasikini.

Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Morogoro waliohudhuria mafunzo ya elimu ya fedha.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter