Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Mkombozi Method Kashonda amesema gawio la wanahisa wa benki hiyo limeongezeka kutoka Sh. 20 na kufikia Sh. 25. Kashonda ameongeza kuwa malipo hayo yatafuata taratibu zilizowekwa na Soko la Hisa la Dar es salaam (DSE) na yatafanyika kuanzia Julai 6 baada ya taratibu zote kukamilika.
Mwaka jana, ongezeko la amana za wateja ambalo lilichangia kwa kiasi kikubwa katika ufanisi wa benki hiyo lilifikia Sh. 121.12 bilioni kutoka Sh. 102.55 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 18 huku mikopo nayo ikiongezeka kwa asilimia 10.8.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, George Shumbusho ameeleza kuwa benki ya Mkombozi imejipanga kutekeleza miradi mbalimbali katika jamii ikiwemo miundombinu ili kukabiliana na mahitaji ya hivi sasa na hata baadae.