Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla ametoa wito kwa Benki ya NMB kuendelea kubuni huduma rafiki kwa makundi mbalimbali katika Jamii ili kuweza kuwafikia wateja wengi zaidi.
RC Makalla ametoa wito huo wakati wa warsha kwa viongozi wa Serikali wa mkoa huo iliyolenga kueleza fursa mbalimbali zinazopatikana katika benki hiyo ikiwemo mikopo ya riba nafuu.
Hata hivyo, RC Makalla ametoa wito kwa Halmashauri za Mkoa huo kushirikiana na Benki hiyo hususani kwenye kukopa fedha za kuwezesha kutekeleza miradi yenye tija na itakayoongeza mapato kwa Halmashauri.
Aidha RC Makalla ameipongeza NMB kwa kutoa gawio la Sh. bilioni 30.7 kwa Serikali pamoja na ushirikiano mkubwa wanaoonyesha kwa Mkoa wa Dar es Salaam katika kufanikisha masuala ya kijamii ikiwemo elimu, afya, usafi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna amesema malengo matano ya kuandaa warsha hiyo ni pamoja na kuwaeleza faida ya kutumia benki ya hiyo, uwezo wa Benki na utayari wa kufanya kazi.
Malengo mangine ni kutumia fursa ya teknolojia na ubunifu wa benki yao katika ukusanyaji mapato na malipo mbalimbali.
Ameongeza kuwa lengo lingine ni kuomba Halmashauri kushirikiana na Benki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mikopo ya riba nafuu na kuwaomba viongozi hao kuwa mabalozi kwenye kutambulisha bidhaa zao.
Bi. Zaipuna pia amemuhakikishia RC Makalla kuwa benki ya NMB itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mkoa huo katika masuala yote ya kijamii.