Benki ya Standard Chartered imezindua kwa mara ya kwanza huduma mpya katika soko la fedha nchini.
Uwepo wa bidhaa hiyo ni juhudi za benki kulihudumia soko la fedha kwa njia ya mtandao linalokuja juu kwa sasa.
Huduma hiyo inayojulikana kama ‘SC Keyboard Banking’ inatoa nafasi ya matumizi ya mitandao ya simu katika mitandao ya kijamii kupata huduma mbalimbali za kifedha.
Huduma hiyo ni sehemu ya mabadiliko makubwa ya utoaji huduma kwa simu kupitia benki ya kidijitali.
Huduma hii ambayo imezinduliwa nchini Tanzania, ipo nchini Kenya, Uganda na Ghana.
Huduma hii kupitia mitandao ya kijamii ni ya kwanza kwa benki katika bara la Afrika na kwamba zinatarajiwa kupelekwa nchini Botswana, Zambia, Zimbabwe na Nigeria kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Watumiaji wa Huduma hiyo watakuwa na uwezo kutuma fedha kwa muda huo huo na kufanya malipo mengine na kuangalia salio kwa kutumia mtandao wa kijamii au jukwaa.
Upekee wa huduma hiyo ya kidijitali unatokana na ukweli kuwa mtumiaji anaweza kufanya kuwa chaguo la msingi katika simu yake na hivyo kuwa na kasi katika kupata huduma ya kibenki bila kujiingiza katika applikesheni za benki ya kidijitali (SC Mobile App) kupata huduma.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Mkuu wa Wateja wa Kawaida wa Benki hiyo, Bw. Ajmair Riaz, alisema kwamba kuwepo kwa Huduma hiyo ya SC Keyboard Banking ni hatua muhimu katika safari ya kidijitali ya benki hiyo.
Alisema kwamba huduma hiyo imebuniwa kwa kuzingatia maslahi ya wateja ambapo wateja sasa wanaweza kulipa tozo mbalimbali, kuangalia akaunti zao na kusafirisha fedha kupitia mitandao ya kijamii iwe ni kwenye Whatsup, Instagram, Facebook, Messenger au njia ya kawaida ya ujumbe mfupi (SMS).
“Tunataka shughuli hii iwe nyepesi na rafiki na kwamba tupo tayari kuendelea kutumia teknolojia ya kisasa ili kuwezesha shughuli za kibenki kuwa za kisasa zaidi na zinazozingatia mahitaji ya wateja.” alisema.
Naye Mkuu wa Teknolojia katika benki hiyo Bw. Christopher Vuhahula, alisema wataendelea kuimarisha ubunifu katika teknolojia ya dijitali katika huduma za fedha.
Balozi wa bidhaa hiyo Vanessa Mdee amesema amefurahishwa mno kujihuisha na huduma hiyo na kuwataka mashabiki wake kutumia huduma hiyo kurahisisha maisha yake.
“Kama wapenzi wangu mnavyojua, mimi ni mtumiaji mzuri wa simu lakini SC Keyboard Banking ina niruhusu kuendelea kuchati huku naendelea na shughuli zangu za kifedha, imefanya maisha kuwa rahisi zaidi” alisema Vanessa.
Katika masuala ya dijitali Standard Chartered’ ina aplikesheni inayoitwa “SC Mobile Tanzania App” kwa kupitia Playstore au AppStore.