Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad ametaja benki za serikali ambazo zimekuwa zikifanya biashara kwa hasara kwa miaka mitatu mfululizo. Prof. Assad ametaja benki hizo kuwa ni Benki ya Wanawake Tanzania (TWB), Benki ya Biashara (TIB), Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Benki ya Posta Tanzania (TPB), na Benki ya Twiga.
CAG amesema kuwa benki ya Twiga na TWB zipo chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutokana na benki hizo kuwa na mitaji midogo. Kwa upande wa benki ya TIB, mikopo ya shilingi bilioni 3.69 imefutwa katika mwaka wa fedha 2018/19.
“Nilibaini benki tano za serikali zilikuwa na uwiano wa chini wa mtaji wa msingi na mtaji wa jumla ikilinganishwa na mali zilizoambatana na vihatarishi na mali zilizo katika hali hatarishi zilizo nje ya urari wa kimahesabu kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Benki na Taasisi za Kifedha ya mwaka 2010 na mwongozo wa BoT wa Agosti 5, 2015”. Imesoma Ripoti ya Prof. Assad.
Aidha ripoti ya CAG pia imeeleza kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imekuwa ikitekeleza asilimia kubwa ya shughuli zake kuu kwa ufadhili wa wahisani, jambo ambalo amedai linaweza kuathiri shughuli za msingi za ofisi hiyo.