Home BENKI Bilioni 1.2 zafadhili CRDB Marathon kwa miaka minne

Bilioni 1.2 zafadhili CRDB Marathon kwa miaka minne

0 comment 190 views

Zaidi ya Tsh. Bilioni 1.2 zimetolewa kufadhili CRDB Bank International Marathon kwa kipindi cha miaka minne.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amebainisha hayo Agosti 18, 2024 wakati wa Kilele cha CRDB Bank International Marathon 2024 iliyofanyika katika viwanja vya The Green, OysterBay jijini Dar es Salaam.

Ameeleza kuwa, fedha zote zilizotolewa katika kipindi cha miaka minne kwa ajili ya kufadhili programu hizo ni zaidi ya Bilioni 1.2 za Kitanzania. “Hakika ubunifu wa CRDB Bank International Marathon umekuwa na matokeo chanya na mchango mkubwa kwa Taifa letu hususani katika sekta ya afya,” amesisitiza Dkt. Biteko.

Amesema fedha zinazopatikana kupitia Marathon zimekuwa na manufaa makubwa kwa jamii ya Watanzania ikiwemo Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambayo imekuwa mnufaika kwa watoto zaidi ya 400 kupata Masada wa matibabu ya magonjwa ya moyo katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

“Nichukue fursa hii kuwapongeza sana Benki ya CRDB kupitia Taasisi yenu ya CRDB Bank Foundation kwa ubunifu huu mkubwa wa kuandaa CRDB Bank International Marathon na jinsi mnavyoiendesha kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali pamoja na washiriki mmoja mmoja na kupata matokeo makubwa mkidhihirisha msemo wa Kiswahili wa “Haba na haba hujaza kibaba,” amesema Dkt. Biteko.

Ametoa rai kwa wadau wote wa Sekta ya Michezo kutumia Marathon zinazofanyika kupeleka tabasamu kwa watu wenye uhitaji mbalimbali kwa kuwawezesha kupata huduma muhimu za kijamii zikiwemo huduma za Afya.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (mwenye koti jeusi) akishiriki CRDB Marathon jijini Dar es Salaam.

Kuhusu michezo, amesema Serikali inatekeleza miradi kadhaa kuhakikisha vijana wengi nchini wanashiriki katika michezo kwa kutambua kuwa michezo sio tu burudani bali ni ajira.

“Sehemu ya mipango ambayo inatekelezwa ni pamoja na kuratibu na kuyaboresha mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA ili kuwaandaa vijana wetu kuanzia wakiwa shule za msingi na sekondari,” ameongeza Dkt. Biteko.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Bank ya CRDB Abdulmajid Nsekela amesema CRDB Marathon imefanyika kwa msimu wa tano na kuwakutanisha washiriki zaidi ya 10000 kutoka mataifa mbalimbali.

Aidha marathon hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwa kusaidia Sekta ya afya kupata vifaa tiba na wenye uhitaji kupatiwa matibabu.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter