Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Benard Dadi amesema benki hiyo imezindua mfumo mpya wa malipo ya fedha kwa njia ya kielektroniki ambao utawezesha utumaji wa huduma za kifedha kutoka taasisi moja kwenda nyingine. Dadi amewaambia waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mfumo huo kuwa, utaondoa udanganyifu katika taasisi za fedha na vilevile kurahisisha utumaji. Mbali na hayo, pia utasaidia benki hiyo kupata taarifa za kifedha katika kila benki badala ya kusubiri kupelekewa taarifa hizo na taasisi za benki.
“Mfumo huo utasaidia kuonyesha kila muamala unaofanyika katika kila kampuni nyingine, kwa hiyo kutusaidia kujua miamala ni mingapi kwa siku, kwa mwezi, kwa mwaka, kuleta udhibiti ndani ya BoT, badala ya kwenda kwenye kampuni kwenda kuomba taarifa, hizo taarifa tutakuwa nazo, tutajua serikali inapata ushuru kwa kiasi gani kwa usahihi zaidi bila kutegemea mpaka ifike mwisho wa mwezi ndio tupewe taarifa kujua serikali imepata ushuru kiasi gani”. Amesema Mkurugenzi huyo na kuongeza:
“Vyote hivyo vitarahisishwa sana kupitia mfumo huu na kufanyika miamala utakuwa unachukua muda mfupi ndani ya sekunde mbili au tatu kumfikia mteja na pia itasaidia kupunguza gharama. Mfumo huu unajengwa ndani ya miezi 18 na utatumia wataalamu kutoka BoT”. Amesema Dadi.