Benki ya CRDB imekabidhiwa kibali cha kuuza Hatifungani ya Kijani “Kijani Bondi” ya miaka 5 yenye thamani ya dola za marekani Milioni 300 sawa na Sh. Bilioni 780 na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).
Kibali hicho cha kutoa hatifungani ya kijani kimekabidhiwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, Nicodemus Mkama kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela aliyeambatana na Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Ally Laay katika hafla iliyofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam Agosti 24, 2023.
Kibali hicho kinaifanya Benki ya CRDB kuwa ya kwanza nchini kutoa hatifungani ya kijani, na ya kwanza kwa ukubwa Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Taarifa ya CRDB inasema Kijani Bond itarahisisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kufadhili miradi rafiki kwa mazingira na kuchochea ufikiaji wa Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG).