Benki ya DTB-Tanzania, imezindua huduma tatu za Prepaid Card, DTB Wakala na Merchant Point of Sales (POS), ili kuwafikia wateja walio mbali na matawi yao. Mwenyekiti wa Bodi ya benki hiyo, Abdul Samji amesema lengo la benki hiyo ni kuwekeza zaidi kwenye teknolojia na kuhakikisha wateja wake wanapata huduma bora.
“Kwa kuzindua huduma kupitia mawakala, wateja wetu watapata huduma za kibenki moja kwa moja kupitia mawakala 110 ambao wamesambaa nchi nzima. Huduma zinazopatikana kwa kupitia mawakala wetu ni kuweka fedha, kutoa fedha na kuangalia taarifa fupi za miamala”. Ameeleza Samji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na benki hiyo, kadi za Pre-Paid ambazo zipo kwenye mfumo wa MasterCard zina uwezo wa kubeba fedha takribani aina kumi za kimataifa zikiwemo Dola za Marekani, Yaun ya China, Paundi, Rupee na Randi ya Afrika Kusini. Huduma hiyo inawafaa wafanyabiashara wanaosafiri nje ya nchi, wanafunzi wanaosoma nje pamoja na watalii,
Huduma ya Merchant Point of Sales (POS) inamuwezesha mteja kufanya malipo kwenye mashine za Visa na MasterCard kwenye maduka makubwa maarufu, hotelini na vilevile katika maduka ya kawaida ili kumuondolea mteja adha ya kutembea na fedha nyingi kila wakati.
Hadi sasa benki hiyo ina matawi 28 nchini kote na kati ya hayo 14 yapo jijini Dar es salaam.