Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Benki ya Biashara nchini (NBC) kuongeza wigo wake wa utoaji huduma ili kuwafikia wananchi wengi zaidi. Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Theobald Sabi jijini Dar es salaam na kuongeza kuwa, wakati huu ambao serikali imekuwa ikihamasisha wananchi kujikita zaidi katika kilimo, benki zinapaswa kuwasogezea huduma karibu zaidi ili kuwapa nafasi ya kutunza wanachokipata kwa usalama na uhakika zaidi.
“Ninatoa wito kwenu mpanue wigo katika utoaji wa huduma zake hapa nchini ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kuhifadhi fedha zao katika eneo salama”. Amesema Waziri Mkuu.
Aidha, Majaliwa pia ametumia fursa hiyo kuipongeza NBC kwa jitihada zake mbalimbali za kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuwawezesha wananchi, kupitia mikopo inayotolewa kwa wajisiriamali wadogo ili kuongeza mitaji yao ya biashara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa NBC ameishukuru serikali kwa kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara, ambapo amesema kwa mwaka wa fedha uliopita, wamefanikiwa kutengeneza faida na kwamba wanatarajia kutoa gawio kwa mara nyingine.