Meneja Mkurugenzi wa Benki ya NIC kitengo cha biashara Rahim Kanji amesema benki hiyo imetambulisha rasmi huduma yake ya malipo ya bima kwa lengo la kuwawezesha wateja wake ambao ni wanachama wa Shirika la Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) kulipia michango hiyo kidogo kidogo.
“Tunaona uwezo mkubwa sana kwenye magari ya usafirishaji abiria na pia ya mizigo, huduma hii mpya ya bima inatupa nafasi ya kipekee kukuza biashara yetu kwa upande mmoja na kwa upande mwingine kuwarahisishia malipo wateja wetu”. Ameeleza Kanji.
Meneja huyo amedai kuwa kutokana na umuhimu wa huduma hiyo, benki hiyo imeweka timu maalum kwa ajili ya kusimamia huduma hiyo kwa wamiliki wa mabasi kote nchini na kuongeza kuwa mkutano na TABOA ni hatua ya msingi wakiendelea na mchakato huo wa kutoa huduma sio tu kwa wateja wao bali kwa taifa zima.
“Benki yetu haiachi kutafuta namna ya kuendelea kuboresha na kuzindua huduma mbalimbali zinazotimiza mahitaji ya aina tofauti”. Amesema Meneja huyo.