Meneja wa NMB anayeshughulikia dawati la China, Agnes Mulolele amethibitisha taarifa kuwa benki hiyo imelenga kupeleka huduma ya kubadilisha fedha za kigeni katika maeneo yote ambayo watalii 343 kutoka China watatembelea kwa muda wa siku tano.
“Ni kweli tumeamua kusogeza huduma karibu ili kuweza kuwahudumia watalii wote katika huduma za kifedha. Huduma hiyo ya kubadili fedha za kigeni itawahusu zaidi wafanyabiashara na watu maarufu, wawekezaji kutoka katika kampuni 27, waandishi wa habari 40, maofisa wa serikali ya China na mawakala wa kampuni za utalii waliokuja kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii”. Amesema Meneja huyo.
Pamoja na hayo, Mulolele amesema wamelenga kusogeza huduma hiyo kwa watalii ikiwa ni moja ya namna ya kuisaidia nchi katika kufikia malengo yake ya kimaendeleo na kuboresha mazingira ya utalii hususani katika suala zima la kubadilisha fedha.
Aidha, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameeleza wakati akiwapokea watalii hao kuwa Tanzania na China zina historia ndefu. Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii Hamis Kigwangalla amebainisha kuwa serikali inazidi kufanya mambo makubwa hususani katika sekta ya utalii.