Na Mwandishi wetu
Katika juhudi za kujiimarisha na kuwa karibu zaidi na wateja wao, Benki ya NMB imefungua matawi saba kwa mpigo katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu. Matawi hayo yamefunguliwa katika mikoa ya Njombe, Songwe, Mbeya, Katavi na Rukwa ambapo baadhi ya matawi yaliyofunguliwa ni pamoja na NMB Kasumulu, NMB Mkwajuni, NMB Uyole, NMB Laela, NMB Kalambo na NMB Wanging’ombe. Matawi hayo mapya yanafanya jumla ya matawi ya benki hiyo katika ukanda huo kufikia 207 nchi nzima.
Katika hafla ya uzinduzi wa Tawi la NMB Uyole mkoani Mbeya, Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Badru Iddy amesema benki hiyo inatazamia kusogeza huduma zake karibu zaidi kwa wananchi na kwamba eneo ambalo benki hiyo imefunguliwa lina wafanyabiashara wengi ambao ndiyo wateja wakubwa. Ameongeza kuwa tawi hilo litatoa huduma zote za kibenki kama matawi mengine ya benki hiyo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makalla amewaambia wananchi wakati wa uzinduzi huo kuwa, wafungue akaunti na kuitumia benki hiyo kwa kuwa hata serikali ina hisa ya asilimia 32 NMB. Ameongeza kuwa kila ambapo serikali imepeleka huduma za kijamii benki hiyo hufuata hivyo ameshauri wananchi kujitokeza kwa wingi na kuitumia huduma za benki hiyo.