Siku chache baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutangaza kuwa serikali inadhamiria kufufua upya kilimo cha michikichi, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetangaza mkakati wa kusaidia kutatua changamoto zilizopo ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo mkoani Kigoma na kutekeleza kwa vitendo maagizo ya serikali.
Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Japhet Justine amesema benki hiyo inalenga kutekeleza mpango wa kuendeleza zao hilo kwa kuongeza uzalishaji wa mbegu bora. TADB pia inashirikiana na Wakala wa Mbegu (ASA) ili kuwezesha wakala hao pamoja na wadau wengine kuzalisha miche ambayo gharama yake itakuwa nafuu.
“Lengo la benki ni kuwawezesha wakulima wadogo wadogo kupata mikopo yenye masharti nafuu kupitia vyanma vya ushirika ili waweze kumudu gharama zote zitakazochochea uzalishaji wa zao hilo mkoani Kigoma”. Amedai Mkurugenzi huyo.
Zao la michikichi ni moja kati ya mazao ya mafuta ambao hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Kigoma, Tanga na Mbeya huku mkoani Kigoma ukiongoza kwa kulima kwa wingi. Inakadiriwa, kuwa eneo linalofaa kwa kilimo cha zao hilo ni hekta 114,018 huku eneo linalotumika kwa sasa likiwa ni hekta 19,640.9 pekee ambalo huzalisha takribani tani 31,750.90.