Benki Kuu ya Tanzania (BOT) inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kushusha riba hadi asilimia 9 .
Gavana wa BOT Profesa Florens Luoga amesema hayo kwenye kongamano la uwasilishaji wa machapisho ya wataalam wa fedha kuelekea mahafali ya kwanza ya Chuo cha Benki Kuu Tanzania yanayotarajiwa kufanyika leo, Novemba 25, 2022.
Amesema hadi sasa benki nchini zinatoa mkopo kwa riba ya kati ya asilimia 11 na 13.
“BoT tumepunguza gharama za uendeshaji wa benki nchini kutoka asilimia 70 hadi 50 na kuanzisha mfuko maalum wa kukopesha mabenki kwa sharti la kukopesha fedha kwa watu kwa riba isiyozidi asilimia 10,” Amesema Luoga.
Ameeleza kuwa “riba sio inapungua kwenda asilimia 10, ilikuwa asilimia 22, tumefanya kazi mpaka imeenda asilimia 17, lakini BOT inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha kuwa riba inaenda hadi kwenye dijiti moja.”
Profesa Luoga, pia amezitaka benki zote zinazokopesha katika shughuli za kilimo ziwe zinafuatilia maendeleo ya miradi hiyo.
Amesema wananchi wa Tanzania zaidi ya asilimia 90 ni wakulima au wanafanya shughuli ndogo ndogo za biashara
Aidha, amesema thamani ya fedha ya Tanzania inaendelea kubakia katika hali ya utulivu kwa hatua thabiti haswa wakati huu nchi inapopitia changamoto za uviko-19 na changamoto za vita za Urusi na Ukraine.
Amesema chuo cha benki kuu na kushirikiana na vyuo vingine wataendeleza juhudi katika kufanya utafiti wa usimamizi wa fedha.