Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kanda ya Dar es salaam imetoa amri kwa benki ya Ecobank Tanzania Limited kuwalipa wafanyakazi wake 25 fidia ya takribani Sh. 974,586,300 milioni kwa kuwaachisha kazi mwaka jana. Shauri la mgogoro huo lilifunguliwa na wafanyakazi hao baada ya kujiridhisha kuwa kanuni na sheria hazikufuatwa wakati wakiachishwa kazi.
Baada ya msuluhishi wa mgogoro huo Alfred Massay kusikiliza hoja kutoka pande zote mbili, alitupilia mbali hoja za utetezi wa mdaiwa na kujiridhisha kuwa wafanyakazi hao waliondolewa kazini pasipo taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria kufuatwa. Massay ameamuru benki hiyo kuwalipa wafanyakazi wote 25 malipo ya kukatishwa kazi, posho ya likizo ya kila mwaka pamoja na madeni ya malipo ya likizo.
Benki ya Ecobank ilipunguza wafanyakazi Juni 2017 kwa madai ya kupunguza gharama za uendeshaji kutokana na hali mbaya ya kifedha na matumizi ya teknolojia. Benki hiyo pia ililazimika kufunga baadhi ya matawi yake kutokana na hali hiyo.