Ofisa Mtendaji Mkuu wa masuala ya uchumi kutoka kituo cha AlHuda cha Benki ya Kiislamu, Muhammed Zubair Mughal ametoa wito kwa watanzania kuchangamkia benki za kiislamu ili kuboresha maisha na kupiga vita umaskini. Mughal ametoa ushauri huo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuhusu umuhimu wa benki hiyo ambapo ameeleza kuwa, benki hiyo inalenga kuwasaidia maskini pamoja na wafanyabiashara.
“Benki za kiislamu hazina riba, zipo kwa ajili ya watu wote waislamu na wakristo, hivyo watanzania ni fursa kwao kuzikimbilia kwa lengo la kujikwamua kimaisha na umaskini”. Amesema Ofisa Mtendaji huyo.
Mbali na hayo, Mughal pia amezungumzia mtazamo hasi wa jamii kuhusu benki za kiislamu na huduma wanazotoa na kueleza kuwa watu wengi wamekuwa wakihususha na Sharia na kuomba serikali kuziingiza benki za kiislamu kwenye sera ili nazo zipate nafasi ya kukuza uchumi wa taifa.