Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Kitengo cha Malipo ya Kadi wa Benki ya Barclays, Philbert Casmir ameshauri watanzania kutumia kadi za kielektroniki za benki maarufu kama ATM wakati wanafanya manunuzi yao ya kila siku ili kupunguza kutembea na fedha taslimu, jambo ambalo amedai litapunguza uhalifu kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Casmir amesema kuwa benki ya Barclays inashirikiana na Kampuni ya GSM hivi sasa kama jitihada mojawapi ya kupeleka huduma zao karibu zaidi na wateja, pia kukuza ushirikiano wa benki hiyo na makampuni ya ndani.
Mbali na hayo, ameongeza kuwa wateja wa benki hiyo hivi sasa wanaweza kupata punguzo la asilimia 15 wakifanya manunuzi katika maduka ya GSM na ametoa wito kwa wateja wa Barclays kutumia nafasi hiyo.
Benki ya Barclays ilipata tuzo ya Visa Agile mwaka jana ambayo inatambuliwa kama benki bora ya Tanzania ambayo imefanikiwa katika matumizi ya kadi. Benki hiyo ina wateja takribani 70,000 mpaka sasa ambao hutumia ATM katika manunuzi yao ya kila siku.