Benki ya Dunia kupitia Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Bella Bird imetangaza ufadhili wa takribani Sh. 1.357 katika miradi mbalimbali inayohusu sekta ya elimu hasa elimu ya awali na sekondari kuanzia mwezi ujao. Bird ametangaza ufadhili huo Ikulu jijini Dar es salaam wakati akifanya mazungumzo na Rais John Magufuli. Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imeeleza kuwa miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa katika mazungumzo hayo ni pamoja na maendeleo ya miradi inayofadhiliwa na benki hiyo hapa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu, Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa thamani ya miradi inayotekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia hapa nchini imefikia Sh. 10.186 trilioni na kuongeza kuwa maendeleo ya miradi hiyo ni mazuri. Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na Tehama, uboreshaji usafiri jijini Dar es salaam, barabara, maji na uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme.
Pamoja na hayo, Bird pia amesema kuwa, wanakamilisha maandalizi ya ufadhili wa miradi mingine ya sekta ya elimu itakayogharimu Sh. 1.357 trilioni na kuweka wazi kuwa maandalizi hayo yatafikia tamati mwezi ujao.