Balozi wa Kenya nchini Tanzania Mh. Dan Kazungu amehimiza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili kwa maslahi ya kiuchumi kwa pande zote mbili ili kuleta maendeleo katika nchi hizo.
Balozi huyo akiongea na pesatu.com kuelekea maadhimisho ya miaka 55 ya uhuru wa Kenya alisisitiza umoja na mshikamano baina ya pande zote ambao utaimarisha uhusiano na kukuza biashara baina ya nchi hizo jirani ambazo zinachangia mipaka ambayo ni muhimu kibiashara.
Waziri huyo wa madini zamani wa Kenya pia aliahidi kuendeleza umoja na ushirikiano hasa mipakani ili kuimarisha mazingira ya biashara baina ya nchi mbili hasa baada ya kufunguliwa kwa kituo cha pamoja cha biashara katika mpaka wa Namanga kilichofunguliwa na maraisi Dk. John Magufuli na Uhuru Kenyata.
Pia alikumbusha jinsi nchi hizi jinsi zinavyotegemeana tangu enzi za kale wakati wa harakati za kupigania uhuru akikumbuka jinsi Mwalimu Nyerere alivyoshirikiana na Jomo Kenyata kuhakikisha Kenya inapata uhuru na jinsi ambavyo taifa la Kenya linathamini utu na wema wa Nyerere kwa taifa hilo “Nyerere alijitahidi kuhakikisha Kenya na Tanzania zinapata uhuru siku moja japo haikufanikiwa ila wema wake tunaukumbuka”.
Balozi alimshukuru Raisi John Magufuli kwa kumpatia hati ya kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mkoani Dodoma kitu ambacho kitarahisisha utendaji kazi wa balozi huyo nchini baada ya serikali kuhamia Dodoma rasmi. Pia alimpongeza kwa kudumisha ushirikiano na Kenya licha ya changamoto mbalimbali zilizopo.
Licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya wanachama kwa ajili ya maslahi ya pande zote hasa kiuchumi na kibiashara baina ya nchi na nchi. Pia aliwakumbusha wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa za masoko nchini Kenya ili kukuza uwiano wa biashara uliofikia Dola za kimarekani milioni 213 kwa mwaka 2016.