November 26, 2021 Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) inarejesha safari zake kati ya Tanzania na Kenya.
Hatua hiyo, pamoja na mambo mengine inatarajiwa kuimarisha biashara baina ya nchi hizi mbili za Ukanda wa Afrika Mashariki.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Tweeter, Rais wa Tanzania Samia Suluhu ameipongeza ATCL kwa kuandika “naipongeza ATCL kwa kupanua huduma za safari za ndege zake ndani na nje ya nchi ikiwemo kurejesha safari za Dar es Salaam – Nairobi, Kenya zitakazoanza Novemba 26, 2021.
Ni matarajio yangu kuwa tutaendelea kuiunga mkono ATCL ili ikue zaidi na kutimiza matarajio ya Watanzania”.
Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Ladislaus Matindi anaeleza kuwa kurejeshwa kwa safari hizo kutaongeza mahusiano na biashara baina ya nchi hizo mbili.
“Tunatazamia kuimarisha mahusiano baina ya Tanzania na Kenya ambapo tumekuwa marafiki wa kuamainiana wa muda mrefu,” amesema Matindi.
Nauli ya safari moja itakuwa Dola za Marekani 210 sawa na takribani Tsh 480,000.