Naibu Waziri Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Zainab Katimba amemwelekeza mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba mkoa wa Kagera kuhakikisha ujenzi wa soko la kisasa la Muleba unakamilika ndani ya miezi sita.
Pia amemwelekeza kukamilisha haraka hatua za manunuzi na kupata mkandarasi wa ujenzi wa soko hilo ambapo takribani Tsh bilioni mbili zitatumika katika ujenzi huo.
Maelekezo hayo ya Katimba ameyatoa kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mohamed Mchengerwa kwenye mkutano wa hadhara wa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi Agosti 11, 2024 Muleba Mjini wakati akijibu kero za wananchi na kueleza mafanikio ya serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Ujenzi wa soko hilo upo katika hatua ya manunuzi na kupata mkandarasi na akipatikana mkandarasi inabidi ajenge ili wananchi waanze kutumia soko hili kwa maana lilikuwepo lakini linaboreshwa.
Na kwa hatua hii naomba kumsisitiza mkurugenzi aweze kuharakisha taratibu za manunuzi na mkandarasi apatikane na ndani ya miezi sita ajenge soko hilo ili wananchi waanze kulitumia kwasababu fedha ipo bilioni mbili,” ameeleza Katimba.
Amemsisitiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Muleba kuwa soko hilo litakapokamilika na kuanza kutoa nafasi kwa wafanyabiashara lizingatie nafasi za wafanyabiashara waliopisha eneo hilo kwaajili ya ujenzi ili waendelee na shughuli zao.
Aidha, Katimba amewaeleza wananchi wa Wilaya ya Muleba kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya serikali ya awamu ya sita kumekuwa na ongezeko la bajeti katika sekta ya barabara kupitia TARURA kutoka Tsh bilioni .3 hadi Tsh bilioni 4.3 kwa mwaka ambayo ni ongezeko la zaidi ya asilimia 230 ya bajeti kwa mwaka.
Balozi Dkt. Nchimbi amehitimisha ziara yake katika mkoa wa Kagera kwa mkutano wa hadhara katika wilaya ya Muleba akielekea mkoa wa Geita akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali.