Ni wajibu wa mfanyabiashara kufanya kila jitihada kuilinda biashara yake na kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa. Madai, na kesi kila wakati katika biashara au kampuni si jambo zuri kwako na linaweza kusababisha biashara ikose wateja, na watu wasitake kufanya biashara na wewe.
Hivyo hizi ni baadhi ya njia ambazo unaweza kutumia kuilinda biashara au kampuni yako:
Kila unachokifanya na kusema kinaweza kuathiri biashara yako kwa namna moja au nyingine hivyo unatakiwa kuwa makini na maneno au vitendo vyako. Kuwa makini na watu unaofanya nao biashara kwani unaweza kuhisi kuwa watu hawaoni mambo unayofanya lakini si kweli, hivyo epuka kufanya biashara na watu ambao wanaweza kusababisha jamii ikufikirie tofauti, au watu ambao wanaweza kusababisha serikali ikuhoji. Pia epuka kudanganya, kufanya matendo au kuongea maneno yanayoweza kuleta malumbano katika jamii.
Ajiri mwanasheria. Watu wengi huwa hawaoni umuhimu wa wanasheria hadi matatizo yakitokea. Ni muhimu kwa wafanyabiashara au wamiliki kuwa na mwanasheria sio tu kwa ajili ya matatizo bali hata kupata ushauri kabla ya kufanya mambo yanayohusu biashara. Hakikisha mwanasheria wako ana ujuzi kuhusu sheria na kanuni zilizopo katika eneo husika la biashara yako. Kabla ya kuajiri mwanasheria, hakikisha unafanya utafiti ikiwa ni pamoja na kuomba ushauri kwa wafanyabiashara wengine, kuuliza watu waliowahi kufanya kazi na mwanasheria huyo ili ufanye maamuzi sahihi na kuilinda biashara yako.
Tofautisha mambo binafsi na ya biashara. Watu wengi hupenda kuchanganya masuala yao binafsi na ya biashara hivyo tatizo likitokea pande zote mbili huathirika, muda mwingine hii inaweza kupelekea kuifunga biashara. Hivyo ili kuepukana na hatari hiyo jitahidi kutofautisha masuala binafsi na ya biashara ikiwa ni pamoja na kutofautisha vifaa vya kazi na biashara, fedha binafsi na za biashara ndio maana unashauriwa kujilipa ili kuweka mali binafsi ikiwa biashara itapata matatizo au kuweka biashara salama ikiwa kutatokea hatari katika mambo binafsi.
Bima ni muhimu . Mbali na bima ya biashara mmiliki wa biashara anatakiwa kuangalia aina nyingine za bima ambazo zinaweza kusaidia biashara yake ikiwa tatizo litatokea. Moja ya bima muhimu katika biashara ni pamoja na bima ya dhima (liability), hii husaidia kama mteja amepata tatizo katika eneo la biashara na mara nyingi kosa linakuwa sio la mmiliki au wafanyakazi wa biashara husika lakini mmiliki anatakiwa kumlipa au kugharamia jambo husika kwa mfano mteja anaweza kudondoka na akahitaji matibabu hiyo inakuwa ni jambo ambalo hakuna mtu alipanga lakini ndo limetokea na mmiliki anatakiwa kugharamia .
Hakikisha nyaraka zako ziko salama, siku hizi watu wengi wanatumia kompyuta kuhifadhi nyaraka za biashara, hivyo hakikisha ziko salama ikiwa jambo litatokea na unahitajika kuonyesha ushahidi. Hivyo kama unatumia kompyuta basi hakikisha unaweka programu maalum kuepusha hitilafu mbalimbali za mfumo wa kompyuta ambazo zinaweza kusababisha upotevu wa nyaraka. Kama unaweka nyaraka zako katika mfumo wa kizamani basi jitahidi kuziweka katika usalama ili kuepuka majanga kama wizi.
Kwa kufanya mambo haya biashara au kampuni inakuwa salama kwa asilimia kubwa sio katika masuala ya madai peke yake bali hata dhidi ya majanga kama moto, mafuriko n.k.