Home BIASHARA Hatua za kupata alama ya ubora TBS

Hatua za kupata alama ya ubora TBS

0 comment 255 views

Wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa kwa ujumla hutakiwa kuweka alama ya ubora ya TBS katika bidhaa zao. Ni muhimu kwa sababu watumiaji wana haki ya kutumia fedha kuunua bidhaa zenye viwango ili kuepuka majanga yanayoweza kutokea iwapo watatumia bidhaa za chini ya viwango.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) hushughulika na masuala ya viwango na limekuwa likifanya kila jitihada kuhakikisha kuwa bidhaa zilizo chini ya kiwango zinateketezwa.

Mfanyabiashara yeyote kabla ya kupata nembo kutoka TBS hutakiwa kupata barua kutoka Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) inayoeleza shughuli anazozifanya mfanyabiashara husika. Ikiwa mfanyabiashara huyo anauza bidhaa za chakula hutakiwa kuambatanisha taarifa kutoka idara ya afya au Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA). Pia ni muhimu kwa mfanyabiashara kuambatanisha leseni ya biashara yake.

Baada ya kuwa na taarifa hizo mwenye biashara hutuma maombi kwa Mkurugenzi wa TBS, baada ya Mkurugenzi kupata maombi hayo hurudisha majibu kwa muombaji akieleza taratibu na gharama zinazohitajika. Katika majibu huambatanishwa fomu ambayo mfanyabiashara hutakiwa kujibu na kurudisha majibu TBS.

Pia Mfanyabiashara hutakiwa kuambatanisha taarifa zifuatazo; Mtiririko wa uzalishaji wa bidhaa husika, Mfumo wa uongozi unaoelezea kitengo cha udhibiti ubora, Orodha ya malighafi zinazotumika na mahali zinakotoka katika kila bidhaa, pamoja na ramani inayoelekeza jinsi ya kufika kiwandani kwa mfanyabiashara.

Baada ya kurudisha majibu mfanyabiashara hupewa tarehe ambayo TBS watafika katika kiwanda chake kwaajili ya kufanya ukaguzi wa awali na kukagua hali halisi ya kiwanda au eneo ambalo biashara husika inafanyika. Wakaguzi kutoka TBS watafika katika kiwanda na kuchukua sampuli ya bidhaa husika kwa ajili ya kwenda kupima ubora wake. Baada ya kupima ripoti hutolewa kuhusu biadhaa husika.

Majibu kutoka maabara ya TBS yanaweza kumfanya mfanyabiashara apate nembo ya TBS kama bidhaa yake ipo juu ya kiwango na kama ni tofauti na hapo basi TBS husitisha kutoa nembo hiyo na kumuelekeza mhusika kufanya marekebisho na ukaguzi kurudiwa.

Matumizi ya nembo ya TBS hutumiwa na mfanyabiashara kwa mwaka,hivyo kumtaka mfanyabiashara kuifufua upya kila mwaka ili kuendelea kutumia nembo hiyo na TBS kuhakikishwa kwamba kanuni na sheria kuhusu bidhaa zinafuatwa.

 

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter