Home BIASHARA Ingiza kipato kwa kukodisha

Ingiza kipato kwa kukodisha

0 comment 246 views

Biashara ya ukodishaji ni moja kati ya biashara muhimu na kubwa zinzazofanywa na watu wengi duniani. Fasili ya ukodishaji ni kitendo cha kutumia mali ya mtu kwa malipo ya fedha au kumlipa mtu fedha baada ya kutumia mali yake kwa muda uliopangwa kama makubaliano baina ya mteja na mmiliki. Vipo vitu vingi duniani ambavyo vimekuwa ni kawaida kukodishwa kutoka kwa mmiliki kwenda kwa mteja wake. Baadhi ya vitu hivyo ni nyumba, vyombo vya usafiri na kumbi za starehe

Zipo fursa mbalimbali za kiuchumi na biashara zinazotokana na kukodisha . Inawezekana nyingine umezisikia na umewahi kuzifanya lakini pia yawezekana nyingine ndo ukaziona hapa. Hivyo jambo la muhimu ni kufuatilia kwa umakini na kuangalia biashara ipi itakufaa kulingana na uwezo wako wa kifedha lakini pia mazingira uliyopo, kwa sababu moja ya jambo kubwa katika kuanzisha biashara ni kuangalia mazingira uliyopo.

Baadhi ya fursa ya ukodishaji ni kama hizi zifuatazo:

Ukodishaji vitabu

Huduma hii ni nzuri hasa kwa maeneo ya mjini ambayo mfanyabiashara anaweza kuanzisha maktaba yake au duka la vitabu kwa ajili ya kukodisha na kuuza kwa wateja mbalimbali. Mara nyingi huduma za kukodisha huenda sambamba na upangaji wa muda wa kurudisha pamoja na mdhamini endapo mtu aliyekodi mali hiyo hatorudisha. Suala la kuzingatia ni kufanya utafiti kabla ya kuanzisha biashara yako hasa kwa kujua jamii inayokuzunguka ina uhitaji wa vitabu gani. Kama umezungukwa na shule au chuo basi ni vema kununua vitabu vinavyohusu taaluma.

Ukodishaji vifaa vya sherehe

Fursa hii imekuwa ikikua kwa kasi . Mwanzoni ilizoeleka kinachokodishwa kwenye sherehe ni muziki tu, lakini kadri ziku zinavyoenda zimeanzishwa kampuni mbalimbali kwa ajili ya sherehe huku zikishugulika kuanzia upambaji, muziki, chakula na vyombo, mwendesha hafla (MC), na hivyo kutengeneza fursa kubwa ya kujiingizia kipato. Sio lazima kuanza na vyote unaweza kuanza na kimoja hata kwa kuwa MC na baadae ukanunua muziki wako na kumuajiri DJ (Msimamia muziki).

Ukodishaji vyombo vya usafiri

Hapa vyombo vya usafiri vinavyozungumziwa ni pamoja na magari, mabasi, magari ya mizigo, pikipiki na hata meli. Shughuli hii ni fursa kubwa katika maeneo mengi nchini, ambapo zipo kampuni mbalimbali ambazo zimekuwa zikijishughulisha na ukodishaji wa vyombo mbalimbali vya usafiri kwa ajili ya shughuli kama sherehe, misiba, utalii na mikutano. Biashara hii inahitaji umakini katika kuisimamia kwa sababu jambo kubwa litakalomfanya mteja kuvutiwa na vyombo vyako ni pamoja na kumhakikishia usalama wa kutosha, usafi pamoja na historia nzuri.

Ukodishaji nyumba na vyumba

Hii ni moja kati ya biashara kubwa zaidi kufanywa duniani kote. Watu wengi wameweza kuwekeza katika miji mikubwa kupitia majengo. Wapo wanaokodisha vyumba katika nyumba za kulala wageni, nyumba za kupangisha watu wa kawaida pamoja na kwa ajili ya ofisi. Fursa hii inahitaji mtaji wa kutosha kuendana na kiasi cha uwekezaji unaotegemea kuanza. Mara nyingi mjasiriamali anashauriwa kufanya utafiti kabla ya kuanzisha ujenzi kwa kuangalia kama biashara anayotaka kufanya inalipa au la kulingana na eneo husika.

Ujasiriamali na uwekezaji ni masuala yanayoenda sambamba na wapo wengi waliofamikiwa kupitia sekta hizi. Ni muhimu kuchukua tahadhari kabla na baada ya kuanzisha biashara yako ili kufikia malengo uliyojiwekea.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter