Home BIASHARA Kampuni ya Acacia Kuhamishia Vitengo Muhimu Nchini Tanzania

Kampuni ya Acacia Kuhamishia Vitengo Muhimu Nchini Tanzania

0 comment 196 views

Kampuni ya Acacia inaendelea kutekeleza mipango ya kuhamishia vitengo muhimu vinavyohudumia biashara zake za Tanzania – yaani ugavi, mauzo na ulipaji wa mishahara – nchini Tanzania. Vitengo hivi vitahamishiwa jijini Dar es Salaam au, ambapo italeta maana zaidi kibiashara, katika migodi yake iliyopo kanda ya ziwa.

 

Mabadiliko haya ni sehemu ya mpango wetu wa muda mrefu ambapo tunalenga biashara yetu ya Tanzania iongozwe na kuendeshwa na wafanyakazi wa Kitanzania kutokea ndani ya Tanzania. Chini ya mpango huu, Asa Mwaipopo aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa makampuni ya Acacia nchini Tanzania mnamo Februari mwaka huu huku katika ngazi ya migodi, kati ya mameneja 16 katika migodi yote mitatu, 12 ni raia wa Tanzania. Katika kipindi cha miaka mitano tumepunguza nguvu kazi kutoka nje kwa 85% na mabadiliko ya sasa yatapelekea kupungua kwa wafanyakazi waliobakia nje ya nchi kwa zaidi ya asilimia 50.

Katika awamu inayofuata ya mpango wa mabadiliko, maeneo yaliyobakia ya vitengo vya ugavi na mauzo, pamoja na sehemu kubwa ya kazi za kitengo cha mishahara, vitahamishiwa Tanzania ifikapo katikati ya mwaka 2019. Mabadiliko haya yatakapo kamilika itamaanisha kwamba vitengo muhimu vya biashara kwa migodi ya North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi vitapatikana ndani ya Tanzania. Kufuatia mabadiliko haya, wafanyakazi na vitengo vilivyo nje ya Tanzania, watakuwa wakihudumia shughuli za makao makuu pamoja na shughuli za utafutaji madini katika nchi zingine barani Afrika.

Kampuni ya Acacia inaendelea kutekeleza mikakati kadhaa ndani ya kitengo chake cha Ugavi ikiwa na lengo la kuongeza manunuzi yake kutoka kwa biashara za kitanzania katika kipindi cha miezi sita ijayo. Kila wakati Acacia imekuwa na utamaduni wa kutumia huduma za Kitanzania kwanza, inapoleta maana kibiashara, na mpango huo unaunda sehemu ya juhudi ya biashara zetu kukuza manunuzi kutoka katika biashara za Kitanzania. Kulingana na mipango yetu ya sasa, tunategemea kwamba ifikapo robo ya kwanza ya 2019 matumizi katika biashara za Kitanzania yataongezeka kwa wastani wa 10% kwa mwaka. Hii itapelekea matumizi ya kampuni katika biashara za Kitanzania zinazoshughulika na bidhaa na huduma – ukijumuisha vifaa vya ujenzi, mafuta na vilainishi, pamoja na intaneti na huduma za ulinzi – kufikia Dola za Kimarekani 170 milioni. Mathalani, kama mgodi wa Bulyanhulu utarejea katika uzalishaji huko mbeleni, na ukawa unafanya kazi kikamilifu, tunategemea ongezeko kubwa zaidi katika matumizi yetu nchini kwa mwaka. Tangu 2016 hadi sasa, Acacia imetumia Dola za Kimarekani 500 milioni kulipa watoa huduma wa Kitanzania.

Maendeleo haya ya hivi karibuni yanadhihirisha  na kutilia mkazo dhamira yetu ya muda mrefu ya kuchangia uchumi wa Tanzania. Tangu kuanza kwa biashara yetu miaka 15 iliyopita, Kampuni za Acacia na watangulizi wake, zimewekeza zaidi ya Dola za Kimarekani 4 bilioni nchini Tanzania, na nyongeza ya Dola za Kimarekani 75 milioni katika jamii zinazozunguka mgodi na kulipa zaidi ya Dola za Kimarekani 1 bilioni kama kodi na mrabaha. Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, makampuni ya Acacia Tanzania, yamelipa jumla ya Dola za Kimarekani 67.1 milioni kama kodi na mrabaha. Hii inajumuisha Dola za Kimarekani 19.1 milioni katika makadirio ya kodi ya mapato ya kampuni, malipo ya mwisho ya kodi ya mapato ya kampuni kwa mwaka 2017 ya Dola za Kimarekani 4.2 milioni, mrahaba wa Dola za Kimarekani 25.7 milioni, kodi za mishahara zinazofikia Dola za Kimarekani 13.0 milioni na kodi nyingine zinazofikia Dola za Kimarekani 5.1 milioni. Mgodi wetu wa North Mara pekee unachangia takribani Dola za Kimarekani 250,000 kwa siku ikiwa ni kodi na mrahaba kwa uchumi wa Tanzania.

Kulingana na utafiti huru wa Ernst and Young wa mwaka 2017, makampuni ya Acacia yalichangia Dola za Kimarekani 712 milioni katika uchumi wa Tanzania, au takribani 1.5% ya jumla ya Pato la Taifa. Hii ilijumuisha jumla ya Dola za Kimarekani 143 milioni kama kodi na mrabaha iliyolipwa 2017, ikijumuisha kodi ya mapato ya kampuni ya Dola za Kimarekani 34.6 milioni, mrabaha wa Dola za Kimarekani 44.9 milioni, kodi zinazohusiana na mishahara zinazofikia Dola za Kimarekani 46.1 milioni na kodi ya zuio, ushuru wa kuagiza mizigo na kodi zingine zinazofikia Dola za Kimarekani 17.5 milioni.

Asa Mwaipopo, Mkurugenzi Mkuu – Tanzania, alisema: “Sasa tunaona matunda ya mpango wa muda mrefu wa Acacia, wa ushiriki wa wazawa, ambao ni kipaumbele katika jitihada zetu za kuendelea kuchangia katika kuinua uchumi wa Tanzania na kusaidia kufikia malengo ya kujenga uchumi wa viwanda. Kama mshirika wa Tanzania na jitihada za taifa kuelekea Dira ya Maendeleo 2025, tumefanikiwa kuzijumuisha biashara za kitanzania katika mnyororo wetu wa ugavi na kuyajengea uwezo makampuni kuweza kufikia viwango na mahitaji yetu ya kiutendaji hasa katika ngazi ya migodi.”

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter