Home BIASHARA Kanuni ya Pareto inavyokuza biashara

Kanuni ya Pareto inavyokuza biashara

0 comment 212 views

Kanuni au sheria ya 80/20 maarufu kama Kanuni ya Pareto iligunduliwa na mchumi Vilfredo Pareto mwaka 1906. Kutokana na utafiti wake, Pareto aligundua kuwa 80% ya ardhi nchini Italia inamilikiwa na 20% ya watu, katika mtizamo mwingine kanuni hiyo inamaanisha kuwa takribani 80% ya athari hutokana na 20% ya sababu mbalimbali katika kila jambo.

Katika upande wa biashara, unaweza kugundua kuwa 80% ya mauzo hutokana na 20% ya wateja, au 80% ya mauzo hayo hufanywa na 20% ya wafanyakazi. Asilimia zinaweza kubadilika lakini mara nyingi, vitu vidogo huleta matokeo makubwa zaidi.

Kama mfanyabiashara mwenye malengo ya kufanikiwa, ni mambo gani unaweza kufanya huku ukitumia kanuni hii kufikia malengo yako?

Kwanza tambua mambo muhimu machache ambayo yanafanya biashara yako ipate matokeo chanya na kuyafanyia kazi zaidi. Kwa kuweka nguvu ya ziada katika mambo hayo ni rahisi kupata matokeo mazuri kuliko kufanya kila kitu na kwa uwezo wote, kwani inaweza kuwa unaelekeza nguvu na juhudi nyingi katika masuala yasiyo na umuhimu na ambayo hayana faida kubwa.

Kwa upande wa wateja, ni wazi kuwa wateja wapya wanakuja kila siku lakini kuna ile asilimia ndogo ya wateja ambayo hufanya manunuzi na kuleta mapato mengi zaidi kuliko wateja wa muda mfupi. Hivyo unashauriwa kuwazingatia hao na kujua wanahitaji nini ili kuweza kuboresha zaidi bidhaa yako na kuvutia wateja wapya wenye mahitaji kama ya wateja wako wa kila siku (ambao ni asilimia ndogo).

Aidha katika upande wa wafanyakazi, ni dhahiri kuwa ni asilimia ndogo husababisha matokeo makubwa licha ya kila mfanyakazi kufanya kazi yake kwa bidii. Hivyo basi wekeza zaidi kwa wafanyakazi wanaoleta matokeo chanya ili kuweza kufikia malengo ya biashara, pia wahamasishe na wafanyakazi wengine kufanya zaidi ili kuweza kupata faida mbalimbali ambazo wanapata lile kundi dogo (20%). Hii itaongeza ufanisi wa kazi na kuleta matokeo chanya katika biashara.

Katika upande wa teknolojia za kisasa hususani mitandao ya kijamii ambayo inatumika sana na wafanyabiashara, mfanyabiashara anaweza kutumia kanuni hii ya pareto. Kwa kujua wateja wako, itakuwa rahisi kujua ni mitandao ipi ya kijamii inatakiwa kuzingatiwa zaidi ili kuweza kuwafikia wateja kwa wingi hivyo hakuna ulazima wa kujitangaza katika kila mitandao. Kuweka juhudi katika mitandao michache kunaweza kukufanya upate wateja zaidi na matokeo mazuri zaidi kuliko kujitangaza katika kila mitandao ya kijamii. Kama bidhaa au huduma unayotoa inawalenga wafanyakazi basi ni unaweza kufanya matangazo katika mtandao wa kijamii kama LinkedIn na kupata matokeo mazuri.

Mbali na hayo, kanuni hii haimaanishi kuwa asilimia lazima iwe 80/20, bali asilimia zinaweza kubadilika inaweza kuwa 90/10, 70/30 nk lakini siku zote mambo madogo au machache huleta matokeo kwa asilimia kubwa. Hivyo mtu yoyote anaweza kutumia kanuni hii kujifunza na kubadilisha mwenendo katika biashara ili kufikia malengo na kufanikiwa.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter