Wote tutakubaliana kwamba changamoto zinakuja na kero mbalimbali. Japokuwa tunajua kuwa ni sehemu ya maisha yetu na ni chachu ya maendeleo, hakuna mtu ambaye anaamka asubuhi ya kutamani siku yake iwe na changamoto nyingi. Changamoto humjenga mtu kuwa jasiri zaidi na kuchukua maamuzi ambayo yanaweza kubadili kila kitu.
Sekta ya ujasiriamali na biashara na ujumla ina changamoto nyingi ambazo ikiwa hujajipanga, unaweza kukata tamaa na kuamua kuachana nayo. Lakini ukiangalia suala hili kwa upande mwingine, watu wengi waliofanikiwa wamesema ni kutokana na mambo mengi ambayo wamejifunza kupitia changamoto walizopitia katika safari zao.
Hizi ni sababu kuu tatu kwanini changamoto sio kitu kibaya kwa wafanyabiashara na wajasiriamali.
Vikwazo vinakupa hamasa ya kufanya kazi zaidi
Unapokutana na vikwazo katika biashara, hali hiyo inakupa motisha ya kufanya kazi mara mbili zaidi ya mtu ambaye hana changamoto zozote katika shughuli zake. Vikwazo ni msukumo mkubwa kwa mtu kujifunza, kuomba msaada kutoka kwa watu wengine, kutafuta ujuzi pamoja na maarifa zaidi ili kuweza kuboresha biashara kwa ujumla.
Vikwazo ni mwalimu mkali, ila mzuri
Ukweli ni kwamba, watu wanajifunza zaidi kupitia vikwazo/changamoto wanazopitia. Hivyo basi ukichukulia changamoto zako kama sehemu ya kujifunza na kuelewa zaidi, unakuwa katika nafasi nzuri ya kuepuka makosa siku za mbele. Japokuwa tunachukia changamoto tunazokutana nazo, hatuwezi kukataa kuwa zinatufundisha mambo mengi ya msingi.
Vikwazo vinaondoa uoga wa kujaribu vitu vipya
Kama unachofanya kila siku kinazalisha changamoto ulizonazo, unakuwa mwepesi zaidi kujaribu vitu vipya ambavyo mara nyingi huleta matokeo makubwa zaidi. Uoga wa kujaribu kitu kipya ni kitu ambacho wafanyabiashara wengi wanakuwa nacho na hivyo wanajikuta wakitumia nguvu nyingi katika hilo badala ya kutafiti vitu vingine vipya. Unapokutana na changamoto ni rahisi zaidi kujaribu vitu au mbinu nyingine na kupata matokeo mapya.
Mara nyingine unapokutana na changamoto, fikiria sababu hizi na tumia changamoto hizo kujifunza, kujaribu na kuwa bora zaidi katika biashara yako, Vikwazo ni sehemu ya maisha ya kila mtu na hivyo, hatuwezi kuviepuka. Tunachoweza kufanya ni kuviona kama fursa ya kujiendeleza na kujifunza ili kukabiliana navyo ipasavyo hapo baadae ikitokea vimerudi tena.