Home BIASHARA Mo Dewji: Bilionea kijana zaidi Afrika

Mo Dewji: Bilionea kijana zaidi Afrika

0 comment 115 views

Mfanyabiashara maarufu hapa Tanzania Mohammed Dewji ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) amesema hivi karibuni kuwa ana mpango wa kuteka ukanda wa Afrika Mashariki kibiashara kwani kuna soko kubwa lenye wastani wa watu milioni 160.

Dewji alizaliwa Mei 08 mwaka 1975 huko Singida na baada ya kumaliza elimu yake ya juu huko Marekani mnamo mwaka 1998 alirejea nchini ili kufanya kazi katika kampuni hii ambayo ilikuwa ikiendeshwa na baba yake hapo awali. Katika jarida la Forbes Africa mwaka 2017 Dewji ametajwa kuwa bilionea kijana zaidi Afrika na tayari ameshawekeza katika nchi 12 barani Afrika.

MeTL inajihususha na sekta mbalimbali zikiwemo ya kilimo, viwanda, uuzaji wa nishati za bidhaa za petrol, usafirishaji na usambazaji wa bidhaa pamoja na chakula na vinywaji. Kampuni hii inachangia pato la taifa kwa asilimia 3.5. Biashara zote zinazoendeshwa chini ya kampuni hii zimetoa ajira kwa watu 28,000 kote nchini. Dewji ambaye hivi sasa utariji wake unafikia Dola za Kimarekani 1.52 bilioni analenga kutoa ajira zaidi kufikia mwaka 2025.

Dewji amepanga kuwekeza zaidi katika nchi za Burundi, Uganda na Rwanda kwa upande wa Afrika Mashariki, lakini amesema hatoishia hapo. Nchi nyingine anazotarajia kuwekeza ni Malawi, Msumbiji, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Bilionea huyo ameongeza kuwa viwanda vya nguo ni sekta muhimu kwa uwekezaji hasa kwa nchi kama Tanzania, Msumbiji, Zambia na Ethiopia ambapo kuna pamba za uhakika.

Kwa hivi sasa, Dewji anatarajia kuongeza vituo vya usambazaji wa bidhaa za kampuni yake ambayo kwa sasa ina vituo zaidi ya 100 na magari 2000. Ameongeza kuwa METL inaongoza kwa usambazaji hapa nchini. Ameshauri Rais wa Tanzania kuboresha miundombinu ya usafirishaji ikiwemo huduma za bandari ili nchi yetu iendelee kupiga hatua zaidi kimaendeleo.

Mbali na kuwa mfanyabiashara maarufu hapa nchini, Dewji pia amesaidia sekta mbalimbali katika jamii kwa kutoa misaada. Amesaidia miradi ya afya, elimu, michezo, maji pamoja kilimo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter