Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Hamisi Kigwangalla anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya uzinduzi wa mkakati huo sambamba na viongozi wengine waandamizi kutoka serikali na pamoja na wadau wa utalii hapa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari jijini Dares Salaam mapema hii leo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mpango huo Bw Mkumbwa Ally alisema mpango huo unaojulikana kama Domestic Tourism Promotion Initiative (DTPI) unalenga kutangaza utalii wa ndani kwa watanzania pamoja na raia wa kigeni kuhusu vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini.
“Ni mpango unaohusisha juhudi mahsusi katika kusaidiana na serikali kukuza utalii wa ndani na kupunguza athari za janga la Corona kwenye sekta hii muhimu.’’ Alibainisha Bw Mkumbwa.
Mkakati huo wenye kauli mbiu ‘Utalii Mpya.Fursa Mpya’ unaratibiwa kwa pamoja baina ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT) na kampuni ya Real PR Solutions ya jijini Dar es Salaam.
Alisema hafla hiyo fupi itahusisha pia ushiriki wa viongozi waandamizi wa serikali na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii wakiwemo Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO), Chama cha watoa huduma za utalii wa ndani (TLTO) na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
Wengine ni pamoja na Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS),Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro, Taasisi ya Sekta binafsi, Chama cha wamiliki wa hoteli pamoja na wadau wengine.
“Zaidi pia tumewaalika Waziri wa Viwanda na Biashara , Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Waziri wa Afya kutokana na michango yao katika ustawi wa sekta ya utalii hapa nchini .” Alisema.
Alitaja baadhi ya mambo muhimu kwenye kampeni hiyo ambayo yatatekelezwa kwa awamu kuwa ni pamoja na Mafunzo kwa vijana kote nchini ili waweze kunufaika na mnyororo wa thamani katika sekta ya utalii ikiwemo kuongoza watalii, mafunzo ya huduma kwa wateja katika hoteli na migahawa, vyombo vya usafiri na ujuzi wa kufungua kampuni za utalii.
“Tunatarajia mafunzo haya yatawanuisha vijana zaidi 100,000 hususani wale wasio na ajira ili waweze kutambua fursa zilizopo kwenye sekta ya utalii na wazitumie vizuri.’’ Alisema Mkumbwa ,.huku akiitaja mikoa itakayoanza kunufaika na mpango huo kuwa ni pamoja na mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Mwanza, Geita, Kagera, Simiyu, Mara na Shinyanga.
Alisema katika kuupamba mkakati huo kutakuwa na uhusishwaji wa matukio mbalimbali ya kimichezo na burudani ili kuvutia walengwa zaidi wa mpango huo.
“Mkakakati huu unahusisha matukio mbalimbali yanayolenga kusaidia ukuaji wa sekta ya utalii nchini na kukuza uchumi wa ndani, lakini pia kuisaidia serikali na wafanyabiashara kuamsha tena biashara zilizokuwa zimezorota kufuatia janga hili la Corona na hatimaye tukuze uchumi wa nchi,’’ alisema Mkumbwa.
Alisema tahadhari zote za kiafya zitachukuliwa kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona katika matukio yote yaliyomo kwenye mpango huo.