Na Mwandishi wetu
Katika mkutano wa pamoja kati ya Benki ya Dunia (WB), Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) na Mamlaka ya Manunuzi na Umma (PPRA), Makamu wa Rais wa TCCIA Octavian Mshiu amesema kuna haja ya kusaidia kampuni zilizopo nchini ili zipate fursa ya kukua na kutambulika zaidi.
Mshiu ameshauri serikali kubana sheria zake ili kufanya kampuni kubwa za kigeni ambazo zinapata zabuni za miradi mikubwa kushirikiana na sekta binafsi za nchi husika kama ambavyo nchi za Afrika Kusini na China wanafanya, kwani mara nyingi kampuni za ndani hushindwa kufika vigezo vilivyowekwa na WB.
Ameongezea kuwa kwa kufanya hivyo taifa litapata ujuzi na teknolojia ambayo itasukuma kampuni za ndani kuelekeza kazi kubwa siku zijazo. Hivi sasa, kampuni kubwa huagiza asilimia 60 hadi 70 ya mahitaji ya ujenzi kutoka nje ya nchi hivyo fedha yote inaishia kwenda nje huku nchi ikiwa hainufaiki. Hivyo kuna umuhimu wa serikali kuangalia upya suala hili ili manunuzi yaweze kufanyika hapa nchini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa PPRA, Dk Lawrence Shirima ameshauri kampuni za Tanzania kujiimarisha kwani ushindani umekuwa ukiongezeka kutokana na uwepo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambao umepelekea nchi wanachama kuleta makampuni ambayo yamejipanga vema.