Waziri wa Biashara na Viwanda Zanzibar, Amina Salum Ali amesema serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Biashara na Viwanda ipo katika mchakato wa kuandaa tamasha kubwa la tano la biashara visiwani humo linalotarajiwa kufanyika tarehe 02-15 Januari 2019. Waziri Amina amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa, tamasha hilo linalenga kuwaunganisha wazalishaji, wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda na kuonyesha matunda ya kazi zao wanazofanya kwa ushirikiano na kuitangaza Zanzibar kibiashara, kiutalii na vilevile kiuchumi.
Waziri huyo amesema tamasha hilo lina lengo la kuadhimisha sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ambapo taasisi mbalimbali zitapata fursa ya kutangaza biashara na huduma wanazotoa huku tamasha hilo pia likitengeneza fursa kwa vijana ili waweze kuonyesha vipaji vyao vya ubunifu na mambo ya asili na kuunda kamati ambayo itaweza kuwatambua wabunifu.
Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri Amina, dira ya tamasha hilo ni kufanya visiwa vya Zanzibar kuwa kituo cha kibiashara, masoko na viwanda vinavyozalisha kwa wingi ili kukuza uchumi endelevu kufikia mwaka 2020.
“Tuacheni kupenda vya wenzetu na kudharau vyetu, tuvithamini vyetu kwani navyo vina hadhi kubwa vinavyozalishwa kwetu ikiwemo sukari ya mahonda, juisi na hata mboga mboga”. Amesema Waziri Amina.