Home BIASHARA TANESCO yafanya mabadiliko kubana matumizi

TANESCO yafanya mabadiliko kubana matumizi

0 comment 122 views

Kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji huku likikabiliwa na makusanyo hafifu, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeamua kujifunga mkanda kukabiliana na hali hiyo ambayo imesababisha shirika hilo kuyumba kiuchumi. Taasisi hiyo ya  serikali imeamua kufanya mabadiliko makubwa ya kiuendeshaji kuanzia makao makuu mpaka ofisi zake za kanda na mikoa ili kukabiliana na hali ngumu ya kifedha ambayo pia imeathiri sekta binafsi nchini.

 

Katika mabadiliko yanayotarajiwa kufanywa hivi karibuni, shirika hilo linatazama kupunguza idadi ya wafanyakazi hasa wale wa dharura na kazi maalumu, kusitisha malipo ya muda wa ziada na safari za mara kwa mara mpaka kibali cha Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo hasa kwa safari zinazozidi siku kumi (10).

 

TANESCO pia imelazimika kusitisha mafunzo ya ziada na kujiendeleza kielimu kwa wafanyakazi huku pia matumizi ya magari kwa maofisa na wafanyakazi yakitakiwa kufanyiwa marekebisho ambapo gari moja litatumiwa na maofisa wasiopungua watatu kwa uelekeo mmoja.

 

Mabadiliko hayo pia yameikumba Idara ya Mahusiano ambapo misaada kwa jamii (CSR) imesitishwa huku matangazo ya redio na televisheni nayo yakisitishwa hadi hapo hali ya kifedha itakapotengemaa.

 

Shirika hilo kwa sasa limeamua kujikita katika kuongeza makusanyo kwa kuzuia wizi wa umeme na ubadhirifu wa fedha kwa wafanyakazi washirika hilo huku likijikita zaidi kuhakikisha mabadiliko hayo yanaenda sambamba na kupunguza kukatika kwa umeme na kuongeza usambazaji wa umeme vijijini.

 

TANESCO licha ya kuwa taasisi ya kiserikali inakabiliwa na kushuka kwa makusanyo hali iliyopelekea kuongezeka kwa deni ambapo kwa mwaka mmoja takribani Sh.140 bilioni zimeongezeka huku makusanyo yakishuka chini kwa takribani Sh.227 bilioni.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter