Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema hayo na kuongeza kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa na kikao na mawaziri ili kutafuta suluhisho.
Mwigulu amesema “tayari Mheshimiwa Rais ameshaguswa na jambo hili amesikia maoni ya Watanzania wote na amesema tuyafanyie kazi jambo hili. Vilevile Waziri Mkuu ameitisha kikao kitakachofanyika kesho (Julai 20) kuendelea kupitia jambo hilo hilo.”
Amesema Serikali imesikia kilio cha wananchi na kuna mambo watakayoyafanyia kazi na mengine wataendelea kuwaelimisha wananchi.
Ameeleza kuwa “tumepokea maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa uelewa zaidi kwa maana ya uelimishaji zaidi ili kuwa na uelewa wa pamoja, ikiwa pamoja na viwango vinavyokatwa, yupi anayekatwa, ukataji wakati wa kutoa na mantiki ya jambo hili zima kwa ujumla,” amesema.
Hata hivyo, amesema kwa kuwa jambo hilo ni la kisheria zilizopitishwa na Bunge, utekelezaji wake utakuwa kwenye kanuni.
“Utekelezaji wake unaangukia kwenye kanuni za ambazo ni za Waziri na zinaangukia sehemu yangu Wizara ya Fedha na Wizara ya Tehama,” amesema.
Huku akitaka sheria ziheshimiwe, Waziri Mwigulu ameonya watu wanaopotosha jambo hilo na kuwataka wananchi kuwa watulivu.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile amesema Wizara yake imekuwa ikikusanya maoni kuhusu tozo hizo na itayafanyia kazi.