Kamishna wa Kodi za Ndani kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Elijah Mwandumbya amesema mamlaka hiyo itaendelea na zoezi la kufanya ukaguzi wa matumizi za mashine za kutolea risiti za kielektroniki zinazofahamika zaidi kama EFD, ili kuhakikisha kila mfanyabiashara anatoa risiti za EFD na kulipa kodi stahiki kama ilivyoagizwa na serikali.
Mwandumbya amesema hayo alipofanya ukaguzi wa kushtukiza katika maduka yaliyopo eneo maarufu la Mlimani City jijini Dar es Salaam. Kamishna huyo amewataka wafanyabiashara kuacha kutumia sababu ya ubovu wa mashine za EFD kwa kuwa mashine hizo tayari zimerekebishwa na sasa zinafanya kazi vizuri bila tatizo lolote.
“TRA haitakubali mfanyabishara anaeonyesha barua kama sababu ya kutokutoa risiti ya EFD, tatizo la mashine lilikwisha, ni wajibu wa wafanyabiashara kutoa risiti”. Amesema Mwandumbya.
Kamishna Mwandumbya amesisitiza kuwa wafanyabiashara wote wanaostahili kutoa Risiti za EFD wanapaswa kufanya hivyo kwa kila mauzo wanayofanya kwani tatizo la mashine lilishughulikiwa na halipo tena.