Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Richard Kayombo amesema mamlaka hiyo imefanikiwa kukusanya Sh. 7.9 trilioni kwa kipindi cha miezi sita ya mwaka wa fedha 2018/19 ikilinganishwa na Sh. 7.8 trilioni zilizokusanywa kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha wa 2017/18.
Kayombo amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa, makusanyo ya Desemba 2018 yaliongezeka kuzidi makusanyo ya miezi yote ambapo TRA ilikusanya jumla ya Sh. 1.63 trilioni.
“Mbali na makusanyo hayo ya mwezi Desemba, katika mwezi Novemba 2018 TRA ilikusanya jumla ya Shilingi trilioni 1.21 na mwezi Oktoba 2018, zilikusanywa jumla ya Shillingi trilioni 1.29. Nachukua fursa hii kuwashukuru walipakodi wote kwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari na wakati”. Amesema Kayombo.
Aidha, kama jitihada mojawapo ya kutatua kero na malalamiko mbalimbali ya walipakodi, Kayombo ametangaza kuwa, uongozi wa TRA umeamua kufanya siku ya Alhamisi kuwa siku maalum kwa ajili ya mameneja wa mikoa pamoja na wilaya wa TRA nchini kuwasikiliza walipakodi na kutatua changamoto wanazokumbana nazo.
“Pamoja na kutenga siku hiyo maalum, tumeanzisha kituo cha ushauri kwa walipakodi kwa mkoa wa Dar es salaam ambacho kipo katika jengo la NHC kwenye makutano ya mtaa wa Samora na Bridge kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuwa karibu na walipakodi. Tumeanza kwa Dar es salaam lakini vituo hivi vitaendelea kufunguliwa katika mikoa mingine nchini”. Ameeleza Kayombo.