Ni muhimu kwa kila mmiliki wa biashara kujua hali ya soko katika tasnia anayojihusisha nayo ili kujua kama malengo ya biashara husika yatatimia au la. Hii husaidia kufanya mfanyabiashara kutengeneza mipango ya kukuza biashara husika na kuepuka kupoteza muda na fedha katika biashara isiyo na soko.
Hivyo basi, Uchambuzi wa SWOT ni nini?
SWOT ni kifupi cha Strength (nguvu), Weakness (udhaifu), Opportunities (fursa) na Threats (vitisho). Hii ni aina ya uchambuzi ambayo humsaidia mfanyabiashara kukuza mkakati wake wa kibiashara kwa kulinganisha sababu za ndani(nguvu na udhaifu) na nje(fursa na vitisho) ambazo zinaweza kuathiri biashara (kuilletea faida au hasara).
Kupitia mchanganuo huu mfanyabiashara hujua hali ya muda huo ya biashara yake na maboresho yapi yafanyike ili kuweza kukuza biashara yake na kutimiza malengo ya biashara kwa ujuma.
Hatua ya kwanza ya kutengeneza uchambuzi huu ni kuunda gridi ambayo itakua ikionyesha vipengele hivyo vinne.
Kwamfano, gridi inaweza kuanza na maelezo yanayoeleza (strength)Nguvu za biashara ambao mtu anaeunda gridi hii anaweza kueleza mambo mazuri kuhusu biashara husika, huduma na ujuzi wa kipekee unaotolewa, uzoefu, mambo bora yanayofanyika katika kampuni husika ikilinganishwa na washindani, nk.
Pia katika kipengele za(weakness)udhaifu, taja vizuizi vya maendeleo katika biashara, rasilimali na ujuzi ambao haupo katika biashara, mambo yanayokuufanya utumie fedha nyingi, mambo ambayo unafikiri yanakushinda na mengineyo kutokana na biashara yako.
Katika upande wa (opportunities)fursa, taja mambo ambayo unaweza kuboresha, mambo ambayo yanaweza kukusaidia kufikia malengo na maono ya biashara, wateja wapya ambao unaweza kuwafikia, nk.
Kwenye kipengele cha (threats)Vitisho, unaweza kutaja mambo ambayo yanaweza kukuharibia biashara yako, mambo ambayo washindani wako wanafanya na wewe haufanyi, mabadiliko ambayo hujaboresha katika biashara yako, unawafikia wateja lengwa, na mengine mengi.
Ili kutathmini ipasavyo uchambuzi huu inashauriwa kuangalia kwanza nguvu zilizotajwa na kuweza kuona ni mambo gani yanaweza kuboreshwa zaidi katika kipengele hiki. Kwani siku zote kuwekeza zaidi katika nguvu ulizo nazo kutakusaidia kufanikisha michakato mbalimbali katika biashara na kutimiza maono.
Pia katika udhaifu, ni muhimu kujua shida au udhaifu unatoka wapi ili kuweza kujua namna sahihi ya kuweza kushughulikia kila tatizo kulingana na uhusiano. Kwamfano unaweza kuwa una udhaifu wa kuwafikia wateja wengi kutokana na aina ya usafiri unaotumia kuwafikia hivyo unaweza kufikiria njia mbadala ya kuweza kuwafikia wateja wako bila kuathiri mtiririko wa fedha.
Sawa katika kila biashara huwa kunakuwa na vitisho mbalimbali, lakini mfanyabiashara makini anatakiwa kuangalia kama vitisho hivyo vinahusiana na nguvu au udhaifu uliopo katika biashara ili kuweza kujua kama anaweza kufanya mabadiliko au la.
Aidha kuhusu fursa, inashauriwa kuangalia fursa za muda mfupi na mrefu zilizopo katika biashara ili kuweza kupanga mipango madhubuti ya kuzitumia fursa hizo ipasavyo ili kuweza kuingiza mapato zaidi.
Ieleweke kuwa, uchambuzi huu hautoi jibu la changamoto au udhaifu uliopo katika biashara bali kupitia uchambuzi huu mfanyabiashara hupata mfumo ambao husaidia kuunda majibu. Hivyo si vibaya kufanya uchambuzi huu kila baada ya muda mfano- mara moja kwa mwaka ili kujua kama malengo ya biashara yako yanatimia au la.