Mtakwimu Mkuu wa serikali ya Zanzibar, Mayasa Mahfoudh Mwinyi amesema ni muhimu kuongeza maarifa na uelewa wa takwimu katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwani kufanya hivyo kutasaidia ukusanyaji na upatikanaji wa takwimu ambazo zitatumika kupanga mipango ya maendeleo ya taifa. Mwinyi ameeleza kuwa, ili kuhakikisha takwimu sahihi zinapatikana kwa ufasaha, Ofisi hiyo imejipanga kuimarisha takwimu za kawaida wakishirikiana na taasisi husika.
Mtakwimu huyo ameeleza kuwa hivi sasa, bado takwimu za kawaida zinakosekana hivyo Ofisi hiyo imedhamiria kuzisaidia taasisi wataalamu na nyenzo nyingine ili kufanikiwa kuziweka takwimu vizuri na kutumika bila mashaka ya aina yoyote.
“Takwimu zikiwa vizuri zitaturahisishia kufanya tafiti zilizokuwa hazina masuala mengi, bado tuna changamoto katika hili”. Amesema Mwinyi.
Kuhusu suala la mgongano katika utoaji takwimu kwa wadau mbalimbali, Mtakwimu huyo amesema ofisi hiyo inafanya kazi na taasisi husika ili kuondoa tofauti zinazotokea baina ya pande hizo mbili pindi takwimu zinapotolewa.
“Hata Rais wetu alizungumzia hili, kinachofanyika sasa ni kuhakikisha takwimu zote zinapitia ofisi yetu na kutolewa baada ya taasisi husika kuzihakiki kiuwiano kabla ya kutolewa”. Amesema Mwinyi.