Home BIASHARA Uhusiano wa Tanzania na Kenya muhimu-Dk. Shein

Uhusiano wa Tanzania na Kenya muhimu-Dk. Shein

0 comment 111 views

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amesema ushirikiano wa kibiashara baina ya mataifa ya Tanzania na Kenya ni muhimu katika harakati za kukuza uchumi na kuendeleza mahusiano yaliyopo. Katika mazungumzo yake na Balozi mpya wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu, Dk. Shein amesema kuna kila sababu ya kuendelea kushirikiana ili kuimarisha sekta za maendeleo hususan biashara.

“Uhusiano huu unaanzia mbali katika historia ambapo Zanzibar ilikuwa kitovu kikuu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki tokea karne ya kumi na tisa”. Ameeleza Dk. Shein.

Mbali na hayo, Dk. Shein amelipokea kwa mikono miwili wazo la Balozi Kazungu la kutaka kuwe na utaratibu maalum wa kushirikiana ili kukuza uchumi na kuinua ustawi wa maisha ya wananchi kutoka pande zote mbili. Rais huyo pia ametumia nafasi hiyo kuipongeza Kenya kwa manunuzi ya karafuu kutoka visiwani Zanzibar, hatua ambayo amedai imesaidia kwa kiasi kikubwa kutokomeza biashara ya magendo iliyokuwepo siku za nyuma.

Kuhusu sekta ya utalii, Dk. Shein amesema kuna haja kubwa ya kuimarisha ushirikiano wa Kenya na Zanzibar ili kuipeleka mbali sekta hiyo ikiwa Kenya imepiga hatua katika masuala ya utalii ikilinganishwa na Zanzibar.

Kwa upande wake, Balozi Kzungu ametoa pongezi kwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kufuatia azma yake ya kukuza mahusiani ya kihistoria na kindugu kati ya taifa lake na visiwa vya Zanzibar.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter