Katika hali ya kawaida kampuni au biashara haiwezi kukua na kufikia malengo ikiwa kila mapato yanayopatikana yanatumika hasa katika masuala yasiyokuwa na umuhimu katika biashara. Mara nyingi matumizi makubwa hutokea katika huduma zinazowezesha bidhaa ifike kwa mfanyabiashara na kwenda kwa mteja, ndio maana inashauriwa kwa kila biashara kujijengea utamaduni wa kuchanganua mtiririko wa fedha ili kuweza kujua vipaumbele katika biashara. Hii husaidia huondoa mambo yasiyokuwa na msingi katika bajeti na kuweza kutumia fedha hizo katika masuala yenye umuhimu zaidi.
Baadhi ya mambo ambayo yamewapelekea wafanyabiashara wengi kupoteza fedha nyingi katika biashara zao ni kama haya;
- Ukosefu wa bajeti rasmi, ikiwa huna mfumo maalum wa kufuatilia matumizi ya biashara yako basi tambua kuwa unapoteza fedha nyingi. Kwani si rahisi kwa kampuni kukua kama hakuna ustaarabu wa matumizi na taarifa kamili kuhusu mtiririko wa fedha. Mfanyabiashara makini anatakiwa kuondokana na mazoea ya kusubiria mapato yajayo ili kuweza kusuluhisha gharama za zamani, kwani si kila wakati mambo yatakwenda vizuri ndio maana bajeti ni muhimu.
- Punguzo la bei, hii hutokea wakati wa kujumua mzigo au uzalishaji ambapo wafanyabiashara wengi hukubali kufanya malipo bila kuuliza kama kuna njia mbadala ya ulipaji (kwamfano kwa mkopo), kama mchuuzi anaweza kupunguza bei, au kama kuna wachuuzi ambao wanauza bidhaa hiyo lakini kwa bei ndogo zaidi nk. Masuala kama hayo yamewapelekea wafanyabiashara kupoteza fedha nyingi katika ununuzi wa bidhaa au uzalishaji kutokana na kutofanya utafiti wa kutosha au kutokuuliza maswali sahihi. Hivyo ili kuweza kuacha kupoteza fedha katika biashara, utafiti ni suala la msingi ili kuweza kupata bidhaa za jumla au huduma kwa bei ndogo kisha kupata faida na mafanikio baada ya kuuza kwa wateja.
- Kutokutumia fedha za ziada kufanya utafiti wa kuongeza mapato, fedha za ziada zinaweza kuwa ni zile fedha zinazotokana na punguzo la bei kutoka kwa wachuuzi, na watu wanaohakikisha umepata bidhaa za kuuza kwa faida. Wengi hutumia fedha za ziada katika masuala yasiyo na msingi hali ambayo huwapelekea kutumia fedha ambazo haziko katika bajeti kujaribu mbinu mpya za kuongeza wateja kwamfano kwa kutangaza biashara katika mitandao ya kijamii au vyombo vya habari. Ili kuepusha mkanganyiko katika mtiririko wa fedha katika baishara yako ni vyema kutumia fedha za ziada katika masuala ya msingi ili kuweza kuongeza faida na si vinginevyo. Kwa urahisi gawanya gharama katika makundi matatu; gharama ya vitu muhimu, visivyo muhimu na gharama za anasa ili kuweza kujua fedha za ziada zinatakiwa kuelekezwa zaidi katika kipengele kipi.
Mbali na hayo, mifumo mbadala inatakiwa kuchangamkiwa na kampuni ndogo na kubwa ili kuweza kupunguza gharama na kupata mapato zaidi. Kwamfano, inaelezwa kuwa Kampuni ya Apple ndio kampuni ya kwanza inayoongoza kwa matumizi makubwa ya Nishati ya jua ( solar system). Hivyo kampuni nyingine zinatakiwa kuiga mfano huo, na kutumia mifumo mbadala ambayo haina gharama kubwa kwasababu lengo la kuanzisha biashara ni kupata faida kubwa kwa gharama ndogo za uzalishaji.