Home BIASHARA Utalii ukuze biashara

Utalii ukuze biashara

0 comment 93 views

Tanzania ni moja kati ya nchi ambayo imebahatika kuwa na vivutio mbalimbali vya utalii. Wageni wengi kutoka nchi za nje hufika hapa ili kujionea vivutio tulivyonavyo na kwa kufanya hivyo husaidia kuingizia taifa fedha za kigeni. Lakini wafanyabiashara wadogo, wa kati pamoja na wakubwa wanatumia fursa hizi za utalii kuinua biashara zao. Kupitia sekta ya utalii biashara hapa nchini zinaimarika. Hivyo basi, ni nini kifanyike ili kuchochea biashara kupitia vivutio vyetu vya utalii?

Kwanza watanzania kwa ujumla wanapaswa kuwa mabalozi wa utalii ndani na nje ya nchi. Kuna kila sababu ya kujenga mazoea ya kufahamu kwa undani vivutio tulivyonavyo nchini kwetu na sisi wenyewe kuvitembelea ili kuona umuhimu na kufahamu sekta hiyo kwa undani. Kufanya hivyo inakuwa fursa nzuri ya kukutana na watu mbalimbali na kutangaza biashara au huduma yako moja kwa moja. Kuwa katika mazingira haya pia kunasaidia kufahamu watalii wanahitaji nini kutoka katika soko la Tanzania hivyo inakuwa nafasi nzuri kuwapatia kile wanachohitaji.

Ili kukuza biashara kwa kupitia sekta ya utalii, ni muhimu kwa wafanyabiashara pia kuzingatia viwango vya ubora. Ni vizuri kuhakikisha kuwa bidhaa yako inazingatia ushindani wa kimataifa kabla ya kuitambulisha katika maeneo ya kitalii kwani wateja hawa wakifurahia bidhaa zako wanakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kukutangaza kibiashara wakirudi nchini kwao hivyo kupanua wigo la soko kwako. Wafanyabiashara wanatakiwa kuzingatia ubora katika bidhaa zao ili kujenga mahusiano ya kudumu ya wateja wao ambao pia wanaweza kuvutia wateja wengi zaidi.

Vikundi vya ujasiriamali vitumie nafasi hii kutambulisha biashara zao. Kuwe na desturi ya kuuza bidhaa zao katika vivutio vya utalii. Vikundi hivi vinaweza kuingia mkataba na hoteli au mbuga za wanyama ili waweze kupata fursa za kufanya maonyesho ya kibiashara na kueleza watalii wanaofika hapa nchini na hata ambao ni wazaliwa kuhusiana na kile wanachokifanya. Kufanya hivi mbali na kuwapatia soko la biashara pia kunaweza kufungua milango ya mashirika na taasisi mbalimbali kuwekeza au kuwadhamini na hivyo kuweka biashara zao katika nafasi nzuri zaidi.

Sekta ya utalii ina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi. Japokuwa bado kuna changamoto zinazoikumba sekta hiyo kama vile kukosekana kwa umeme wa uhakika lakini kupitia utalii, watanzania wengi wameweza kupata ajira na kubadilisha maisha yao. Serikali kwa kusaidiana na wadau mbalimbali wa masuala ya utalii wanapaswa kuendelea kuelimisha jamii kuhusu vivutio vinavyopatikana hapa nchini ili sekta hii iendelee kuimarika.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter