Home BIASHARAUWEKEZAJI Mgodi wa Buzwagi washinda tuzo Afrika

Mgodi wa Buzwagi washinda tuzo Afrika

0 comment 146 views

Mgodi wa dhahabu wa Buzwagi umeshinda tuzo ya Afrika kwa ushirikiano wao na wafanyakazi wake kuelekea kufungwa kwa mgodi huo miaka miwili ijayo. Mgodi huo ambao unamilikiwa na Acacia Group ulipokea heshima ya juu katika kundi la Mshahara, Utambuzi na Ustawi wa wafanyakazi katika tuzo za Ushiriki wa Waajiriwa wa Afrika zilizofanyika Afrika Kusini tarehe 14 Juni 2018.

Mwaka jana kampuni hiyo ilitangaza kufunga mgodi wa Buzwagi mwaka 2020 na kuzindua programu yake ya “Hakuna Madhara 2020” kwa lengo la kudhibiti athari za kufunga mgodi huo kwa wafanyakazi wake na jamii inayowazunguka. Programu hiyo inalenga kuhakikisha kuwa hatua za mwisho za kufunga mgodi huo zinafanyika kwa namna ambayo wafanyakazi na wanajamii wanaandaliwa kutafuta fursa nyingine mara baada ya taratibu zote za usindikaji madini kukamilika.

Mkurugenzi Mtendaji wa migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu Benedict Busunzu pamoja na timu yake walihudhuria sherehe za tuzo hizo jijini Johannesburg ambapo aliwapongeza wafanyakazi wa Buzwagi kwa jitihada zao.

“Nimefurahi kuona kazi nzuri inayofanywa na wafanyakazi wa Buzwagi kwa watanzania imetambulika kimataifa,” alisema Busunzu. “Hii inadhihirisha kujitoa kwetu katika kuhakikisha Hakuna Madhara itawagusa watu wetu, biashara yetu na jamii kwa ujumla kuelekea kufungwa kwa Buzwagi 2020.”

Kama sehemu ya “Hakuna Madhara 2020” wanachama wa Buzwagi wamepatiwa taarifa,vifaa na muongozo wa kutafuta kazi au kuanzisha biashara zao mwenyewe mara baada ya mgodi kusitisha huduma. Mafunzo yaliyopewa jina la “Maisha baada ya Buzwagi” pia yamewaleta pamoja wadau mbalimbali katika jamii kama vile maafisa kutoka serikali za mitaa na viongozi wa kimila kama jitihada za kukuza msaada kwa shughuli za mgodi na kuwasaidia kuelewa mabadiliko yatakayowakabili wananchi.

Majaji katika sherehe za  tuzo za Ushiriki wa Waajiriwa wa Afrika walifurahishwa na programu ya “Hakuna Madhara 2020” na jinsi ilivyoenda mbali kuliko kampuni nyingine za madini katika kuhakikisha wanawajali wafanyakazi wake kipindi ambapo mgodi huo unasitisha shughuli zake. Wamesema programu ya  “Maisha baada ya Buzwagi” ni mfano wa kuigwa wa ushiriki wa mfanyakazi katika kipindi kilichokuwa kigumu kwa wale waliokuwa na mahusiano ya dhati na mgodi huo.

“Tunatambua mchango wenu kwa wafanyakazi pamoja na kazi muhimu mnayofanya,” wamesema timu ya tuzo za Ushiriki wa Waajiriwa wa Afrika. “Ilikuwa ni heshima kubwa kwetu sisi kusaidia kutambua watu na  programu zinazostahili kama hii ya kwenu.”

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter