Home BIASHARAUWEKEZAJI Sekta binafsi yachangia maendeleo yaliyopo Tanzania: Majaliwa

Sekta binafsi yachangia maendeleo yaliyopo Tanzania: Majaliwa

0 comment 85 views

Maendeleo yaliyopo nchini Tanzania hivi sasa yametokana na uhusiano mzuri uliopo baina ya Serikali na sekta binafsi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameeleza hayo Julai 23, 2024 wakati akizungumza na wadau wa sekta binafsi nchini kwenye ufunguzi wa maadhimisho ya Wiki ya Sekta Binafsi Tanzania kwa mwaka 2024 yaliyofanyika Super Dome, Masaki, jijini Dar es Salaam.

“Maendeleo tunayoyaona nchini kwetu katika kila sekta yanategemea mchango wa Serikali pamoja na sekta binafsi. Dhamira na maono ya Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuimarisha sekta binafsi ili ihuishwe na kuwa mshindani katika kuleta maendeleo makubwa kwa nchi yetu,” amesema Waziri Mkuu.

Amezitaka Wizara na taasisi za Serikali ziendelee kupokea maoni ya sekta binafsi na kuhakikisha yanazingatiwa katika marekebisho ya sera na sheria za biashara ili kuondoa vikwazo vya urasimu na kuboresha taratibu za usajili na uendeshaji wa biashara nchini kwa kuwezesha upatikanaji wa vibali na leseni kwa haraka na kwa urahisi.

Pia amezitaka wizara zinazohusika na viwanda, biashara na uwekezaji kuhakikisha zina buni mbinu za kukuza na kusaidia biashara ndogo na za kati (SMEs).

“Wekeni mazingira mazuri ya upatikanaji wa mikopo nafuu, mafunzo na ufikiaji wa masoko ili kusaidia biashara ndogo na za kati kukua na kuchangia katika uchumi. Biashara hizi ni sehemu muhimu ya kuimarisha sekta binafsi,” amsema.

Akielezea jitihada ambazo zimechukuliwa ili kukuza sekta binafsi na uwekezaji, Waziri Mkuu amesema Serikali imeimarisha mazingira ya biashara kwa kufanya marekebisho katika sera na sheria za biashara ili kuondoa vikwazo vinavyowakabili wafanyabiashara na wawekezaji.

Amebainisha kuwa “hatua hizi zimejumuisha kuboresha taratibu za usajili wa biashara, kupunguza urasimu, na kuongeza uwazi, kutoa fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, nishati, miundombinu, utalii, viwanda na kuanzisha maeneo maalum ya uwekezaji.”

Amesema Serikali imewekeza katika miundombinu ya usafirishaji, nishati, maji na mawasiliano ambayo ni muhimu kwa shughuli za uwekezaji na biashara.

“Hatua hii inalenga kuimarisha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje,” amesema.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzugumza na washiriki wa hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuasisi falsafa mpya ya kushirikiana na Sekta binafsi ikiwemo kuondoa ukiritimba wa mawazo.

“Rais wetu yeye anaamini na anakiri katika dhana ya kusikiliza sauti na mawazo ya wengine ili kuweka mazingira bora ya mahusiano kati ya Sekta binafsi na Serikali”

Amesema kuwa kupitia falsafa hiyo imeshuhudiwa Rais Dkt. Samia akiendesha vikao vya kubadilishana mawazo mara kwa mara na makundi tofauti ya sekta binafsi yaliyojikita katika sekta mbalimbali kwa kusikiliza changamoto, kujifunza mafanikio na kutengeneza mfumo thabiti na sahihi wa kusonga mbele kwa manufaa ya pande zote mbili.

Naye, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema katika mwaka huu wa fedha, wizara hiyo imeweka vipaumbele sita ambavyo vinalenga kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Kwa upande wake, Mweyekiti wa TPSF, Angelia Ngalula, ameeleza kuwa wanatamani kuona Tanzania inakuwa kitovu cha Afrika kutokana na rasilmali ilizonazo.

“Pia tunatamani kuona biashara nyingi zinarasimishwa na wigo wa walipakodi unaongezwa,” amesema Ngalula.

Ameeleza kuwa wakati TPSF inaanzishwa, ilikuwa na wanachama 33 lakini kwa sasa imefikisha wanachama zaidi ya 500 ambao wanajumuisha vyama vya wafanyabiashara na makampuni makubwa.

Wiki ya Sekta Binafsi Tanzania inaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 25 ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter