Home BIASHARAUWEKEZAJI Tanzania kukusanya bilioni 100 kutoka bahati nasibu

Tanzania kukusanya bilioni 100 kutoka bahati nasibu

0 comment 12 views

Wizara ya Fedha inatarajia kukusanya Sh100 bilioni kila mwaka kutokana na uwekezaji wa Dola milioni 20 za Marekani uliofanywa na kampuni ya ITHUBA Tanzania, iliyopata leseni ya miaka minane kuendesha Bahati Nasibu ya Taifa.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande, alipozungumza katika hafla ya kutambulisha uwekezaji huo.

Amesema amesema Serikali itachukua asilimia 18 ya fedha za washindi, pamoja na mapato mengine yatokanayo na mkataba huo.

“Uwekezaji huu utaimarisha sekta ya bahati nasibu nchini na kuchangia mapato ya taifa, huku ukiwa na manufaa kwa jamii,” amesema Chande.

Ameeleza kuwa, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika michezo ya kubahatisha nchini kwa kuwa ni moja ya chanzo muhimu cha mapato ya kusaidia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Chande amesema kuwa, Serikali inajivunia hatua ilizochukua kufanikisha mradi huo mkubwa wa mabadiliko ya Bahati Nasibu ya Taifa ambayo ni ishara ya matumaini, fursa na maendeleo, ambapo kila tiketi ya bahati nasibu inayonunuliwa, mbali na nafasi ya kushinda, ni mchango kwa maendeleo ya Taifa letu.

Ameongeza kuwa uteuzi wa Kampuni ya ITHUBA Tanzania kama mwendeshaji rasmi wa Bahati Nasibu ya Taifa unaonesha uwezo wao wa hali ya juu na uelewa wa kina wa mahitaji ya Tanzania na uteuzi huo ulizingatia utaalam na uzoefu wa ITHUBA, kama mwekezaji wa kimataifa mwenye rekodi nzuri ya kuendesha biashara ya Bahati Nasibu za Taifa barani Afrika ambako inaendesha michezo hiyo katika nchi ya Afrika ya Kusini, Uganda na nyinginezo.

“Ni imani yangu kuwa ITHUBA imejipanga vyema ili Bahati Nasibu ya Taifa iweze kuendeshwa kwa ufanisi na kuleta mafanikio yaliyotarajiwa na hatua hii inafungua matarajio makubwa katika ufanisi wa uendeshaji wa Bahati Nasibu ya Taifa na ukurasa mpya wa mabadiliko katika sekta ya michezo ya kubahatisha hapa nchini Tanzania” amesema  Chande.

Ameongeza kuwa katika nchi mbalimbali duniani, Michezo ya Bahati Nasibu ya Taifa imeonesha uwezo wa kuleta mabadiliko makubwa kwa kuzalisha mapato ya kusaidia vipaumbele vya kitaifa, na hapa Tanzania, Bahati Nasibu ya Taifa itafuata mkondo huo kwa kuhakikisha kuwa mapato yake yanatumika moja kwa moja kwa manufaa ya taifa, huku ikizingatia viwango vya juu vya uwazi, uwajibikaji, na uadilifu chini ya usimamizi madhubuti wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT).

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter