Home BIASHARAUWEKEZAJI Sheria ya madini ya 2017 yaanza kuzaa matunda

Sheria ya madini ya 2017 yaanza kuzaa matunda

0 comment 156 views

Kufuatia Sheria mpya ya madini ya mwaka 2017 yenye kuzitaka kampuni za madini kuandaa mpango wa matumizi ya fedha za huduma kwa kushirikiana na halmashauri kabla ya kuanzisha mradi, serikali kupitia halmashauri ya Geita kwa kushirikiana na kampuni ya madini ya Geita Gold Mining (GGM) imeanza utekelezaji wa miradi mbalimbali kupitia fedha za huduma za maendeleo ya jamii (CSR).

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa miradi mitatu yenye kugharimu kiasi cha Sh 1.5 bilioni, Mkuu wa mkoa huo Robert Gabrieli amesema miradi hiyo ambayo ni ujenzi wa barabara ya mzunguko wenye kugharimu zaidi ya Sh. 300 milioni, jengo la kisasa lenye vyumba 80 litakalogharimu Sh 1.2 bilioni sambamba na uwekaji taa 150 za barabarani utakaogharimu kiasi cha Sh. 70 milioni amesema kuwa ni mapinduzi makubwa yaliyoletwa na mabadiliko ya Sheria mpya ya madini ya mwaka 2017.

“Mwaka huu GGM watatoa Sh 9.2 Bilioni ambazo ni fedha za huduma kwa jamii zinazotarajia kuleta mabadiliko makubwa ya maendeleo kwa jamii” Amesema Gabrieli.

Aidha Mkuu wa mkoa huyo ameagiza mkandarasi anayehusika kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha na kukabidhi mradi huo kwa wakati kwa kuwa hatomvumilia yeyote atakayekiuka makubaliano yaliyofikiwa.

“Makandarasi wengi wazawa ni wababaishaji wanatusumbua miradi yao inasuasua mimi nasema wazi sitawavumilia” Alisema

Akizungumzia uanzishwaji wa miradi hiyo Msimamizi Mkuu wa miradi ya GGM , Moses Rusasa amesema miradi hiyo ni sehemu tu ya miradi yao ambayo imeanza kutekelezwa. Rusasa amesema fedha za huduma za jamii katika mji wa Geita zimejikita katika kuboresha huduma za afya pamoja na elimu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Geita, Modest Apolnary amesema kuwa jengo la kisasa linatarajiwa kuwa na maduka pamoja na benki na amemtaka mkandarasi aliyepewa zabuni hiyo kukamilisha kwa wakati.

 

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter